WMA yasisitiza ukaguzi matumizi vipimo sahihi

WAKALA wa Vipimo (WMA) umesisitiza kuendelea kufanya ukaguzi wa matumizi ya vipimo sahihi kwenye maeneo ya uzalishaji, maghala yanayouza bidhaa kwa ujumla na masoko ili kukuza uchumi imara, jumuishi na ushindani.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Meneja wa WMA Mkoa wa Dodoma, Saidi Ibrahimu, wakati wa kukabidhi mizani iliyohakikiwa na wakala kwa wafanyabiashara wa Soko Kuu la Majengo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani ambayo huadhimishwa Mei 20 kila mwaka.

Amesema moja ya nguzo za Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni kufikia uchumi imara, jumuishi na shindani, na kuwa hilo haliwezi kufikiwa kama bado kuna uuzaji wa bidhaa bila kuzingatia vipimo sahihi.

“Hatuwezi kuifikia Dira 2050 kama bado kuna watu wanauza bidhaa kwa kutumia makopo au lumbesa au vipimo vingine ambavyo si sahihi. Mtu ananunua gunia la kilo 100 la tangawizi akija kuuza anafanya makadirio au anapanga mafungu. Hapa anajuaje faida yake? Uchumi shindani utakuwa mgumu sana,” amesema.

Ibrahimu alitumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi na wafanyabiashara katika masoko na maeneo ya uzalishaji kutumia vipimo sahihi na kuhakikisha mizani yao inapimwa, huku akisisitiza kuwa wakala utaendelea kufanya uhakiki wa kushitukiza kwenye maeneo ya uzalishaji, maghala na masoko.

Alisema kutotumia vipimo sahihi kunaweza kumfanya mfanyabiashara kupata hasara na mwananchi kuuziwa bidhaa pungufu. Alisisitiza kuwa mfanyabiashara asiyetumia mizani sahihi anapaswa kutambua kuwa adhabu inayomkabili ni faini ya Sh milioni 20 au kifungo kisichopungua miaka miwili jela, au vyote kwa pamoja.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara katika Soko la Majengo, Fred Segamang’ombe, alishukuru Wakala wa Vipimo kwa kutoa mizani kwa baadhi ya wanawake wanaofanyabiashara katika soko hilo, jambo litakalowasaidia kufanya biashara zao kwa tija na faida.

Alisema katika Soko la Majengo kuna wafanyabiashara wengi ambao hawana mizani na wamekuwa wakitumia makopo au kupanga bidhaa chini, hali inayowafanya kuuza bidhaa zao kwa hasara.

“Wafanyabiashara wengi wanachukua mzigo uliopimwa kwa mali kauli, lakini wanapouza wanatumia makopo, kufunga kwenye mifuko au kupanga chini bila kuwa na kipimo sahihi. Siku za mwisho anajikuta anapata hasara na kuishia kuwa na madeni.”

“Siku hizi hakuna biashara ya kukisia. Kuwa na mizani kutawaepusha wafanyabiashara kuonekana kuwa ni matapeli au wanamuibia na kumpunja mteja. Hii itajenga imani kwa wananchi tunaowahudumia na pia tunatunza mazingira kwa kuachana na mifuko tunayoitumia kama vipimo.”

Alisema Soko la Majengo lina wafanyabiashara takribani 4,000 na asilimia 80 ya hao wana mizani ambayo imekaguliwa na kugongwa muhuri wa Wakala wa Vipimo Tanzania.

Awali, mfanyabiashara katika Soko Kuu la Majengo, Khadija Abdallah, alisema wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kutokuaminiwa na wateja wanapotumia vipimo visivyo rasmi kama makopo na mifuko, na kuwa kupewa mizani kutarejesha imani hiyo‎-

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button