Tija kilimo cha korosho inataka matumizi sahihi ya viuatilifu

MATUMIZI sahihi ya viuatilifu ndiyo chachu kufikia uzalishaji unaotarajiwa kupatikana katika zao la korosho nchini na hii ni kutokana na uwepo wa baadhi ya magonjwa yanayoathiri zao hilo yakiwemo ‘bright’ na ‘ubwiriunga.’

Wanasema watalaamu mbalimbali wa kilimo cha korosho na kusisitiza kuwa, ili kukabiliana na changamoto ya magonjwa dhidi ya zao hilo, elimu ni muhimu kwa kila mdau anayehusika na mnyororo mzima wa uzalishaji wa korosho wakiwemo maofisa ugani, wakulima na wadau wengine.

Katika kuhakikisha uzalishaji huo unafikiwa, hivi karibuni maofisa ugani 569 mkoani Mtwara wamepatiwa mafunzo kuhusu matumizi sahihi na salama ya viuatilifu vya zao hilo katika Msimu wa Kilimo wa Mwaka 2025/2026.

Mafunzo hayo yalilenga kukumbusha maofisa hao kuhusu matumizi sahihi na salama ya viuatilifu kwenye zao hilo hasa wanapoelekea msimu wa upuliziaji wa mikorosho katika msimu huo wa kilimo mwaka 2025/2026.

Mafunzo yaliyoandaliwa na Kituo cha Utafiti wa Kilimo Nchini (TARI) Naliendele kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) pamoja na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, yalifanyika Mbawala Chini katika Kata ya Naliendele, Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Baada ya mafunzo hayo gazeti la HabariLEO, limezungumza na baadhi ya washiriki akiwemo Mratibu wa Zao la Korosho katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, Asha Mahamudu anayesema, maofisa ugani hao wamekuwa wakipitia changamoto nyingi katika matumizi ya viuatilifu kwa sababu vipo vitu wanavyovifahamu na vingine hawavifahamu.

“Kama tunavyojua kuna mabadiliko ya hali ya hewa yanatokea na mabadiliko ya matumizi ya viuatilifu, kutokana na mafunzo haya tunawafundisha wakulima wetu namna bora ya kuchanganya viuatilifu,” anasema.

Kwa mujibu wa Asha miongoni mwa mambo muhimu wanayohimiza ni muda sahihi wa kupulizia kwa maana ya muda wanaotakiwa kukaa hadi waende tena kupulizia pamoja na umuhimu wa kuzungukia mashamba mara kwa mara ili kutambua magonjwa na wadudu waharibifu wa mikorosho wanaoweza kutokea kwenye maeneo yao.

Ofisa Kilimo wa Kata ya Magengeni, Rashidi Karim anasema mafunzo hayo ni muhimu kwa maofisa hao ni mwongozo mzuri kwa wakulima wa zao hilo kuongeza uzalishaji. Anasema wanachotarajia kuwaelimisha zaidi wakulima wao wakiwemo wa kata yake, ni matumizi sahihi ya viuatilifu vilivyotolewa bure na serikali.

Mkulima na mkazi wa Mbawala Chini Shangani, Ahmad Hamisi anasema, “Nimefurahi sana kupata mafunzo haya maana kabla ya mafunzo nilikuwa napoteza mazao kutokana na kutokuwa na elimu hii, lakini sasa ninaamini Mungu atanijalia maana changamoto kubwa ilikuwa ya upuliziaji.”

Mtalaamu wa magonjwa na wadudu waharibifu wa zao la korosho kutoka Tari, Stanslaus Lilai anasema magonjwa hayo yamekuwa na usumbufu mkubwa katika zao hilo hususani ubwiri unga ambao kama usipodhibitiwa kwa muda sahihi, unaweza kusababisha hasara kwa asilimia 70 mpaka asilimia 100 ya zao hilo.

Anasema kimelea kinachosababisha ugonjwa huo hutambuliwa kwenye majani kwa kuona ungaunga mweupe, maua ya korosho kwani akishambulia kwa kiasi kikubwa maua hayawezi kufunguka, mabibo kuwa madogo na machafu na huwa yanapasuka, korosho changa huwa chafu hatimaye hudumaa na kushindwa kufikia hatua inavyotarajiwa.

Ugonjwa mwingine hatari kwa zao hilo ni ‘bright’ ambao pia kama usipodhibitiwa kwa mapema, unaweza kusababisha hasara ya asilimia 60 mpaka asilimia 100. Kimsingi wataalamu wanasema zipo njia nyingi za kuweza kuondokana na changamoto hiyo ikiwemo matumizi ya mbegu bora zinazozalishwa na watafiti.

Aidha, njia nyingine zinazoweza kutumika kudhibiti magonjwa hayo (ubwiri unga na bright) ni pamoja na usafi wa mashamba, upogoleaji, kuondoa maoteo yanayopatikana chini ya miti yanayotunza vimelea hivyo.

“Njia nyingine ni kuhakikisha kuna matumizi sahihi ya viuatilifu na njia hii inaweza kupunguza magonjwa hayo kwa asilimia kubwa na pia tumewaelekeza hawa wataalamu kuwa karibu na wakulima ili kuwaelekeza zile njia sahihi tulizokuwa tukishirikishana nao ziwafikie kama zilivyo bila kupunguza au kuongeza,” anasema.

Ofisa Kilimo Mwandamizi wa CBT, Geofrey Mwalembe anasema katika Msimu wa Mwaka 2025/2026, wanaendelea na utoaji mafunzo kwa maofisa ugani hao. Katika awamu ya kwanza, yatafanyika katika mikoa ya Mtwara na Lindi.

Amesema kwa Mkoa wa Mtwara maofisa ugani 245 kati ya hao 569 wanaopatiwa mafunzo ni waliyoajiriwa na CBT chini ya programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) wengine 323 ni waliopo katika ngazi ya halmashauri “Lengo ni kuwajengea uelewa kuhusu visumbufu vya zao hilo ili waweze kufikisha elimu hiyo kwa wakulima katika maeneo yao,” anasema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Tari Naliendele, Bakari Kidunda anasema uzalishaji wa korosho umekuwa ukipanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali na kwamba, moja ya changamoto kubwa
ni utambuzi na udhibiti wa magonjwa na wadudu waharibifu wa zao hilo.

“Hii ni miongoni mwa changamoto kubwa, tukifanya vizuri katika eneo hili tutaongeza uzalishaji wa zao la korosho, tukifanya vibaya kwenye eneo hili moja kwa moja uzalishaji utashuka,” anasisitiza Kidunda.

Lengo la serikali ni kuzalisha tani laki 7 katika Msimu wa Mwaka 2025/2026 na tani milioni moja mwaka 2030, hivyo ili kufikia malengo hayo ni lazima iwekwe mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji ukiwamo utoaji wa
elimu.

Mshauri wa Kilimo Mkoa wa Mtwara, Ally Linjenje anasema serikali imetoa viuatilifu katika mkoa huo na kwamba, vinatakiwa kutumika vizuri ili kuleta na kuongeza tija. Anasema katika mwaka 2025 mkoa huo umepokea tani 21,000 za pembejeo za unga na viuatilifu vya maji lita laki 8.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button