Timu za MKUMBI II, Maboresho ya Kodi zakutana

KATIBU Mkuu wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Tausi Kida, amezikutanisha Timu za Wataalamu wa Kuandaa Mpango wa Pili wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI II) na Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi katika kikao kazi maalum kilichofanyika jijini Dar es Salaam kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujadili mbinu za uboreshaji wa mazingira ya biashara nchini.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Dk Kida amesema kuwa mkutano huo umeandaliwa ili kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya kiuchumi.

Amebainisha kuwa lengo kuu ni kujadili mbinu bora za ushirikiano na sekta binafsi katika kushughulikia changamoto za kikodi na zisizo za kikodi, ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na mazingira bora zaidi ya biashara na uwekezaji pamoja na mifumo imara ya kikodi.

Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi kadhaa wakiwemo Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Balozi Ombeni Sefue, pamoja na Wajumbe wa Tume hiyo. Pia alikuwepo Mwenyekiti wa Timu ya Wataalamu wa MKUMBI II, Profesa Faustine Kamuzora.

Mkutano huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha kuwa mipango ya maboresho ya mazingira ya biashara na mifumo ya kodi inatekelezwa kwa kushirikisha wadau wote muhimu, kwa nia ya kuvutia uwekezaji na kukuza uchumi wa taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button