Tishio la Polio kampeni nyumba kwa nyumba

Mikoa sita yawekewa mkakati

JUMLA ya watoto milioni 3.2 walio chini ya umri wa miaka nane wanatarajiwa kupata chanjo ya Polio itakayotolewa Septemba 21 hadi 24 ,2023 baada ya mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi na moja kupata ugonjwa huo Mei 26,2023.

Mtoto huyo ambaye alitolewa taarifa kutoka Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa uchunguzi wa Maabara ulithibitisha kuwa mtoto huyu ana maambukizi ya virusi cha Polio baada ya kuoneyesha dalili za kupooza kwa ghafla.

Chanjo hiyo itatolewa katika mikoa ya Rukwa, Kagera, Kigoma, Katavi, Songwe na Mbeya.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema watashirikiana Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wadau wa Sekta ya Afya kuendesha Kampeni hiyo.

Ummy amesema kuwa maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Polio yametolewa taarifa pia katika nchi zinazopakana na Tanzania mfano Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia hivyo hali hii inaongeza tishio na hatari ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Polio kwa nchi yetu hususani katika Mikoa inayopakana moja kwa moja na nchi hizo.

“Lengo la kampeni hii ni kuwafikia watoto waliozaliwa baada ya mwaka 2016 ili kuwakinga dhidi ya Kirusi cha Polio aina ya pili (Polio Virus Type 2) kinachoweza kusababisha ulemavu wa kudumu na Kwa Rukwa tunatarajia kufikia watoto 391,883 Kagera 729,387 Kigoma 884,477 Mbeya 614,346 Katavi 227,862 na Songwe 402,643,” Amefafanua Ummy.

Amesema katika Kampeni hiyo kutakuwa na jumla ya timu yenye jumla ya watoa huduma za afya 5,291 kwa Mikoa hiyo itakayofikiwa na zoezi hili ambapo kila timu itakuwa na watoa huduma watatu.

“Timu hizi zitakuwa zinatoa huduma ya chanjo kwa walengwa kupitia vituo vya kutolea huduma za afya, nyumba kwa nyumba, shuleni na maeneo mbalimbali ya mikusanyiko ikiwemo Nyumba za Ibada”. ameeleza Waziri Ummy.

Ametoa rai kwa wazazi na walezi kutoa ushirikiano kwa watoa huduma za afya ili kuwezesha watoto wao kuchanjwa kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba.

Habari Zifananazo

Back to top button