TMDA yajadili ajenda tatu kuimarisha utendaji kazi

BARAZA la Wafanyakazi la Sita la Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) limejadili ajenda tatu kuu zenye lengo la kuboresha utendaji kazi wa Mamlaka, ikiwemo kutoa maoni na mapendekezo kuhusu Mpango Mkakati wa TMDA wa miaka mitano (2026/27–2030/31).
Ajenda nyingine zilizojadiliwa ni Rasimu ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 pamoja na Mpango wa Mazingira, Jamii na Utawala (Environmental, Social and Governance – ESG).
Majadiliano hayo yamefanyika kuanzia Februari 5 hadi 6, 2026 mkoani Morogoro, yakihusisha wajumbe wa Menejimenti na wawakilishi wa watumishi wa TMDA, kwa lengo la kujadili na kufikia mwafaka juu ya masuala mbalimbali ya kitaasisi yenye mchango mkubwa katika kuimarisha utendaji kazi wa Mamlaka.

Akifunga kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Dk. Adam Fimbo, amewashukuru wajumbe wa Baraza kwa maoni yao ya kujenga, akisisitiza kuwa wafanyakazi ni nguzo muhimu ya mafanikio ya Mamlaka.
“Baraza la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu la ushirikishwaji na uwazi katika maamuzi ya taasisi. Mawazo na maoni yenu yamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mifumo ya utendaji na kulinda afya ya jamii,” amesema Dk. Fimbo. Amesema lengo kuu la mkutano huo ni kujadili taarifa za utendaji kazi wa TMDA, kubaini fursa na changamoto zilizopo, pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha mifumo na huduma za Mamlaka.

Kupitia Baraza la Wafanyakazi, TMDA imeendelea kuimarisha mshikamano, uwajibikaji na mawasiliano ya wazi kati ya Menejimenti na watumishi, hali inayochangia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi na bidhaa nyingine zinazodhibitiwa, kwa lengo la kulinda afya ya jamii.
TMDA imesisitiza itaendelea kuthamini mchango wa Baraza la Wafanyakazi kama chombo muhimu cha ushirikishwaji katika maamuzi ya kimkakati na uendeshaji wa taasisi, sambamba na azma ya kujenga mazingira bora ya kazi na kutoa huduma bora kwa jamii. SOMA: TMDA yajipanga mikakati mipya utekelezaji dira 2050



