‘Tunataka wafanyabiashara waone TRA, Tiseza ni washirika’

DODOMA; CHEMBA ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC), imesema maboresho makubwa ya kiutendaji yanafanyika ndani ya chemba kwa lengo la kuongeza thamani kwa wafanyabiashara na kutatua changamoto zao kwa wakati.
Kauli hiyo imetolewa leo Februari 10, 2026 mjini Dodoma na Rais wa TNCC, Vicent Minja , wakati wa kikao kazi cha ndani kitakachofanyika kwa siku mbili na kuongeza kuwa dhamira yao pia ni kuhakikisha wafanyabiashara wanapata uwakilishi imara na taarifa sahihi za fursa.
“Kila tunachokiboresha ndani ya TNCC kina lengo moja kuu kumrahisishia mfanyabiashara mazingira ya kufanya biashara na kupata matokeo bora zaidi.
–
“Hili haliwezi kufikiwa bila ushirikiano wa karibu na serikali pamoja na taasisi zake muhimu kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji Kiuchumi (TISEZA).
–
“TNCC itaendelea kuwa daraja imara kati ya wafanyabiashara na serikali ili kuhakikisha sera, kodi, mifumo ya ukusanyaji mapato, na fursa za uwekezaji katika maeneo maalumu ya kiuchumi vinaeleweka vizuri kwa wafanyabiashara na vinatumika kama chachu ya ukuaji wa biashara,” amesema Minja.
–
Amesema kupitia ushirikiano huo, TNCC inalenga kujenga mazingira ya majadiliano ya mara kwa mara yatakayosaidia kupunguza migongano isiyo ya lazima kati ya wafanyabiashara na mamlaka za udhibiti.
“Tunataka mfanyabiashara aione TRA, TISEZA na taasisi nyingine za Serikali kama washirika wa maendeleo, si kama vikwazo.
“Ndiyo maana TNCC tunachukua jukumu la kuunganisha pande hizi kwa mazungumzo ya wazi, elimu sahihi ya mifumo na taratibu, pamoja na utatuzi wa changamoto kwa njia ya kitaasisi,” amesisitiza Minja.
Kwa upande wake, Meneja Maendeleo ya Biashara wa Taasisi hiyo, Mercy Philipo, ameeleza kuwa kikao kazi hicho kinapitia mifumo, huduma, na mikakati ya taasisi ili kuhakikisha TNCC inakuwa karibu zaidi na wafanyabiashara katika maeneo yote ya nchi.



