Tozo matumizi miundombinu bandari kurudi TPA

DODOMA – SERIKALI imependekeza marekebisho kwenye Sheria ya Bandari ya Mwaka 2004 ili kurejesha jukumu la kukusanya tozo ya matumizi ya miundombinu ya bandari kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amebainisha hayo wakati akiwasilisha bajeti ya serikali bungeni, Dodoma juzi.

“Aidha, mapato yatakayotokana na tozo hizo yatawekwa katika akaunti maalumu ya TPA iliyopo Benki Kuu ya Tanzania na matumizi yake yatafanyika baada ya kuomba na kupata idhini ya Mlipaji Mkuu wa Serikali.

Advertisement

“Lengo la hatua hii ni kuiwezesha TPA kupata fedha kwa wakati kwa ajili ya maboresho ya miundombinu ya bandari na hivyo kuongeza ufanisi wake,” alisema Dk Mwigulu.

Hivi karibuni, wadau wa bandari waliishauri serikali kuiruhusu TPA kuendelea kukusanya tozo itokanayo na huduma za bandari (wharfage) kama ilivyo sehemu zote duniani badala ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao kazi yao ni kukusanya kodi.

Walitoa ushauri huo sambamba na wachumi ikiwa ni miezi michache baada ya wabunge kutoa ushauri huo kwa serikali.

TRA inakusanya zaidi ya Sh trilioni moja kwa mwezi nje ya tozo hiyo ya huduma za bandari ambayo ni Sh bilioni moja kwa mwezi.

SOMA: Serikali yaonya wanaotafuna fedha za umma

Ushauri huo umekuja wakati Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha kuridhishwa na mafanikio iliyopata TPA hadi kuongoza katika taasisi zilizotoa gawio serikalini kwa kutoa Sh bilioni 153.9 katika hafla iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam wiki hii.

Mtaalamu wa masuala ya bandari nchini, Emmanuel Mallya alisema serikali kutoruhusu TPA kukusanya tozo hiyo ni sawa na kuizuia kukua na kukwamisha ongezeko la ufanisi unaoletwa na uwekezaji toka sekta binafsi.

Mallya ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Mawakala wa Meli Tanzania (TASAA), alisema ni vyema TRA ikaendelea na majukumu yake ya kukusanya kodi ambayo sehemu kubwa inatokana na ufanisi wa huduma za bandari.

Wakichangia bajeti ya Wizara ya Uchukuzi hivi karibuni, wabunge walisema ili TRA ikusanye kodi zaidi, inabidi TPA iachwe ikusanye tozo ya huduma za bandari kwa ajili ya kuboresha miundombinu, huduma na usalama bandarini.