TPDC boresheni vitalu vya gesi na mafuta

DODOMA: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amelielekeza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuongeza kasi ya uendelezaji wa vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia, yakiwemo maeneo ya Mnazi Bay Kaskazini, Eyasi Wembere na Songo Songo Magharibi, pamoja na mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia (LNG).
Ametoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa miaka 25 wa TPDC (2024/25 – 2049/50) jijini Dodoma, ukiwa na lengo la kuongeza uhakika wa upatikanaji wa nishati kwa soko la ndani na nje ya nchi.
Katika hotuba yake, Dk. Biteko amesema mpango huo wa miaka 25 ni hatua muhimu katika kuhakikisha rasilimali za mafuta na gesi zinachangia kikamilifu maendeleo ya Taifa. Amesisitiza kuwa sekta ndogo ya mafuta na gesi ina nafasi kubwa katika kuimarisha uchumi wa nchi na hivyo TPDC inapaswa kuhakikisha usambazaji wa gesi unawafikia wananchi wengi kupitia teknolojia kama Mini-LNG na CNG.
Aidha, ameitaka TPDC kujiimarisha kifedha kwa kubuni mifumo ya kibunifu ya utekelezaji wa miradi, kupunguza utegemezi kwa fedha za Serikali, na kuendelea na jitihada za kulipa mishahara kwa kutumia mapato ya ndani. Pia amesisitiza umuhimu wa shirika hilo kushirikiana na kampuni za kimataifa, wawekezaji binafsi na wadau wa maendeleo kwa kuzingatia misingi ya mazingira, jamii na utawala bora (ESG).
Katika hatua nyingine, Dk. Biteko ameagiza TPDC kutoa kipaumbele kwa usambazaji wa gesi kwa matumizi ya kupikia ili kupunguza matumizi ya mkaa na kuni, hatua ambayo itasaidia kutunza mazingira na kupunguza hewa ukaa. Ameipongeza pia bodi ya wakurugenzi na menejimenti ya TPDC kwa juhudi wanazofanya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha nishati katika ukanda huu.
SOMA: TPDC yaanza utafiti mafuta, gesi Ziwa Eyasi
Kwa upande wao, viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Nishati Zanzibar, Shaib Kaduara, na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, wamepongeza mkakati huo wa TPDC na kuutaja kuwa ni dira ya mafanikio ya kiuchumi na kijamii.
Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue, amesema mpango huo ni nyenzo ya utekelezaji wa dira ya maendeleo ya Taifa ya 2050 na Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ukiwa na malengo ya kuongeza ajira, mapato na nishati safi kwa Watanzania.