TPDC yaanza utafiti mafuta, gesi Ziwa Eyasi

SERIKALI kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) chini ya Wizara ya Nishati imeanza kutekeleza mradi wa kimkakati wa utafiti wa mafuta kwenye Bonde la Eyasi Wembere lilipo katika mikoa ya Simiyu, Singida na Arusha.

Utafiti huo ambao ni awamu ya Pili ulianza mwaka 2017, ambapo kwa mujibu wa watalaamu wa TPDC wanaeleza kuwa tangu wameanza awamu hiyo ya utafiti kumeanza kuonekana viashiria vya mafuta na gesi eneo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari, msimamizi wa mradi wa utafiti wa mafuta na gesi katika eneo hilo, Sindi Maduhu amesema mradi huo unatekelezwa ili kutafuta mafuta na gesi katika bonde hilo lenye viashiria vya uwepo wa mafuta na gesi asilia.

Advertisement

SOMA:TPDC yaja kivingine upatikanaji gesi

Amesema Bonde la Eyasi Wembere liko katika Bonde la Ufa la Afrika Mashariki na kwamba bonde hilo linashabihiana na mabonde mengine ya Afrika Mashariki katika nchi za Kenya na Uganda.

Ameeleza kuwa utafiti wa mafuta katika eneo hilo ulianza mwaka 2015 ukidhaminiwa na serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania na kwamba wamefikia hatua za juu zaidi kubaini miamba yenye viashiria vya mafuta.

SOMA: TPDC yakagua mitambo ya gesi

“Mwaka 2015 tukitumia ndege kubaini ukomo wa miamba hiyo na tuliweza kufanya tafiti mbalimbali katikati hapa…tulifanya Utafiti wa Kijiokemia mwaka 2021 na mwaka jana (2023) tulianza Utafiti Kwa njia ya mitetemo ya mfumo wa 2D, njia hii inasaidia kubaini kina Cha miamba pia kubaini mashapo yenye mkusanyiko wa mafuta chini ya ardhi,” amesema.