TPSF yasisitiza matumizi ya teknolojia, ubunifu kumkomboa mwanamke

WAKATI dunia ikiadhimisha Siku ya Wanawake, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imesisitiza kuwa teknolojia kuwa ni nyezo muhimu katika kuchochea usawa wa kijinsia itakayowaweza wanawake kukuza biashara zao.

Akitoa salamu zake za maadhimisho ya siku hiyo, Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula amesema taasisi anayoiongoza inatambua mchango wa wanawake katika mabadiliko ya kiuchumi, mazingira na kijamii kwa maendeleo endelevu huku akisisitiza: “Kuna haja ya kuwawezesha ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili.”

Kaulimbiu ya mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya wanawake ni ‘DigitALL: Ubunifu na teknolojia kwa usawa wa kijinsia.’

“Kuna zaidi ya wanawake milioni 31.7 nchini Tanzania. Idadi hii ina mashiko kwa kuwa kuwawezesha wanawake ni ‘uchumi janja’ na usawa na usawa wa kijinsia unachagiza ukuaji wa uchumi na maendeleo ya binadamu,” amesema.

Ameongeza kuwa wajasiriamali wanakabiliana na changamoto lukuki kwani kwa sasa ni asilimia 7.8 ya wanawake ndio pekee wana uwezo wa kupata mikopo kutoka benki ikilinganishwa na asilimia 22 ya wanaume.

Changamoto nyingine ni masoko, kupata taarifa na ushiriki wao katika uchumi rasmi.

Mwenyekiti Ngalula amesema kuwa ubunifu na teknolojia ni mwarobaini wa kutatua changamoto zinazowakabili wanawake wajasiriamali.

Mwenyekiti wa TPSF ametoa wito kwa serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na taasisi anayoiongoza na kushirikiana ili kuchagiza teknolojia na ubunifu kwa lengo la kuwawezesha wanawake.

Habari Zifananazo

Back to top button