TRA Kariakoo yatoa elimu kuhusu kudai risiti

TRA Kariakoo yatoa elimu kuhusu kudai risiti

MENEJA wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Kikodi Kariakoo, Alex Katundu, amezindua kampeni ya Twende Nao Tukawaelimishe, yenye lengo la kuwaelimisha wanunuzi juu ya umuhimu wa kudai risiti za kielektroniki (EFD), kila wanaponunua bidhaa katika eneo la kibiashara la Kariakoo.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa elimu ya umuhimu wa kudai risiti kwa wanunuzi waliokutwa wamenunua bidhaa bila kudai risiti, Meneja huyo ameeleza kuwa, elimu ya kodi imekuwa ikitolewa mara kwa mara kwa wafanyabiashara, suala ambalo limesababisha wanunuzi wengi kusahau wajibu wao wa kudai risiti.

“Mara nyingi tumekuwa tukitoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu matumizi sahihi ya mashine za kutolea risiti za EFD na sasa hivi tumekuja na mkakati maalumu wa kuwaelimisha wanunuzi juu ya haki yao ya kudai risiti kila wanapofanya manunuzi,” alisema Meneja Katundu.

Advertisement

Amesema kuwa  hilo litafanyika kwa kuwakusanya wanunuzi wote watakaokutwa wamenunua bidhaa bila kuwa na risiti na kupelekwa ofisi ya TRA Kariakoo iliyopo Mtaa wa Lumumba na Kipata, Dar es Salaam kwa ajili ya kuwaelimisha.

“Kwa kuwa wanunuzi hawa wanakutwa katika maeneo mbalimbali ya Kariakoo, hivyo hili linafanyika kwa kuwakusanya wote wanaokutwa wamenunua bidhaa lakini hawana risiti, ambapo wanaletwa hapa ofisini kwa ajili ya kuwaelimisha na kuwaomba wawe mabalozi kwa wengine wenye tabia ya kutokudai risiti,” alifafanua Katundu.

Amesema elimu hiyo itakuwa ikitolewa bure kwa kuwaeleza wanunuzi umuhimu wa kudai risiti, ili kuepuka adhabu ya faini ya Sh 30,000 hadi  Sh milioni 1.5.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *