MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajia kukusanya Sh trilioni 3.49 kwa Desemba, 2024 kiasi ambacho hakijawahi kukusanywa tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo.
Kadhalika, imepanga kuanzia Januari hadi Juni, 2025 kukusanya Sh trilioni 15.27 ili kuhakikisha wanafikia lengo la kukusanya Sh trilioni 31.05 kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mkurugenzi wa Fedha wa TRA, Dinah Edward amesema hayo walipokutana na wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa ajili ya kuwashukuru.
Amesema ushirikiano kati ya BoT na TRA umewezesha kukusanya Sh trilioni 12.94 hadi kufikia Novemba mwaka
huu sawa na asilimia 100 ya mapato ghafi na asilimia 47 ya makusanyo kwa mwaka mzima.
SOMA: TRA yavuka lengo makusanyo Novemba
Ameeleza usimamizi unaofanywa na BoT kwa benki na maboresho ya mifumo ya uhamishaji wa fedha ina mchango mkubwa katika kupanua wigo wa walipakodi na kurahisisha ulipaji wa kodi.
“Usimamizi wa mapato unaratibiwa na TRA lakini ninyi mmekuwa chachu ya kuchangia ufanisi wetu na tunaamini tukiendelea kushirikiana tutafika hatua ya juu zaidi kwa manufaaa ya nchi,”amesema Edward.
Ameongeza kuwa makadirio ya makusanyo waliyojiwekea kwa Desemba hayajawahi kukusanywa tangu kuanzishwa
kwa mamlaka hiyo.
Kwa upande wake, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amesema wanatambua umuhimu wa kulipa kodi, hivyo wao ni mawakala wa kukusanya kodi kutoka kwa wadau na kuwasilisha kupitia mifumo.
Amesema wao wanalipa kodi kutokana na makadirio na maeneo yao na kwamba wana wajibu wa kusimamia sekta ya fedha kuwezesha mamlaka hiyo kuongeza ufanisi na tija katika ukusanyaji wa mapato.
”Tumejipanga vizuri kuwezesha ukusanyaji kodi katika kipindi hiki cha sikukuu kwani mifumo yetu iko vizuri kuruhusu miamala ipite na tutafanya kazi saa 24 kuhakikisha mifumo imara na benki zote zitaongeza muda wa kufanya malipo kuirahisisha mtu anayetaka kulipa,’’ ameeleza.
Amesema kila mmoja anapaswa kutumia mifumo ya fedha iliyopo ikiwemo Mfumo Jumuishi wa Kieletroniki (TIPS), Mfumo wa Malipo Makubwa na ya Haraka (TISS) na Mfumo wa Malipo ya hundi au malipo madogo ya kielektroniki
(TACH).
Amesema kupitia mifumo hiyo, imepunguza gharama ya uhawilishaji fedha na kuwezesha Watanzania kufanya malipo kutoka benki na kupitia simu ya mkononi.
“Niwatoe wasiwasi kwamba akaunti zote za fedha za serikali, za benki na kwenye simu za mikononi ziko salama licha ya majaribio ya mara kwa mara ya udukuzi, hakuna hatari iliyofanikiwa,” amefafanua.