TRA mshindi tuzo uandaaji mahesabu 2023

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeibuka mshindi wa jumla kwenye uandaaji wa hesabu za kifedha zinazozingatia viwango vya kimataifa vya Uhasibu katika Sekta ya Umma (IPSAS) na Sekta za Kibiashara (IFRS).

Tuzo hizo zimetolewa Dar es Salaam na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA).

Kadhalika, TRA imeibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha Taasisi za Serikali (Government Agency Categories) kwenye tuzo hizo.

Advertisement

Akizungumza baada ya kupata tuzo hizo, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Mcha Hassan Mcha amesema tuzo hizo ni uthibitisho wa dhamira ya TRA ya kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na weledi katika matumizi sahihi ya fedha.

Amesema TRA inaandaa taarifa zake kwa kuzingatia viwango vya juu vya kitaalamu katika uandaaji na uwasilishaji wa taarifa za kifedha.

Mcha ameeleza kuwa TRA ina watumishi wenye weledi wa kutosha katika usimamizi bora wa fedha na uandaaji wa taarifa zinazozingatia viwango hivyo vya kimataifa.

“Tuzo hizi ni uthibitisho kuwa TRA tunao watumishi wenye weledi katika kusimamia, kuandaa na kuwasilisha taarifa za fedha kwa kuzingatia viwango vya kimataifa lakini pia ni ishara ya uwazi na uwajibikaji,” ameongeza.

NBAA imekuwa ikiandaa tuzo hizo kila mwaka kwa waandaaji wa taarifa za kifedha zinazozingatia viwango vya kimataifa vya IPSAS na IFRS.