TRA yasisitiza matumizi sahihi risiti za EFD

MAMLAKA ya Mapato Nchini (TRA), imewasisitiza wafanyabiashara kutambua kuwa matumizi sahihi ya Mashine za Risiti za Kielektroniki (EFD) ndio njia sahihi kwa wao kudhibiti ubadhirifu kwenye ofisi zao.

Kamishina wa Kodi za Ndani, Alfred Mregi ameeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Geita mara baada ya watumishi wa TRA kutembelea na kusaidia makundi maalum.

 

Amesema mwamko wa matumizi ya EFD unaendelea kukua, lakini bado kuna watu hawatumii EFD, na wengine wapo wanatumia lakini si kwa usahihi hali inayofanya wafanyabiashara kukosa taarifa sahihi.

“Nitoe wito kwa wafanyabiashara wote kuviona vifaa hivi kwamba ni kwa ajili ya manufaa ya pande zote mbili, kwa sababu unapotumia mashine za EFD, kila unapouza na kutoa risiti, inakupatia tathimini sahihi.

“Lakini inakusaidia kutunza kumbukumbu ya bidhaa zako, kwa hiyo hata kama kuna ubadhirifu mtu hawezi kuufanya kwa sababu kumbukumbu zipo kwenye mashine.” Amesema na kuongeza;

“Watumishi wa TRA tunapokuja kupitia kumbukumbu zako kwa ajili ya kutoza kodi tunakukuta una kumbukumbu sahihi, kwa hiyo kodi ambayo itatozwa pale ni ile inayoendana na mapato yako.

“Lakini wanapokwepa kutumia hizi mashine zina athari kwa biashara zao, katika kukadilia kodi wanaweza wakalalamika kwamba wamekadiriwa kodi kubwa, kumbe suluhu ni kutumia mashine zile.”

 

Amesema mwamko wa matumizi ya EFD na njia rafiki za kudai kodi imewasaidia TRA kukusanya takribani Sh trilioni 23 na kufikia asilimia 97 ya lengo la kukusanya takribani Sh trilioni 24.

Amebainisha mchango wa kodi ndio chachu ya TRA kutoa misaada kwenye kituo cha kulelea watoto cha Kwa Neema House, Gereza la wilaya ya Geita na kituo cha elimu maalum shule ya msingi Mbugani.

Ofisa Mnadhimu wa Mkoa wa Geita, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (SSP) Deogratius Maguza amewapongeza TRA kwa uwajibikaji wanaofanya kuunga mkono juhudi za makundi maalum.

Mkurugenzi wa kituo cha kusaidia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu cha Kwa Neema House mjini Geita, Lucas Matumba amewashukuru TRA kwa msaada na kuiomba jamii kuiunga mkono TRA.

 

Habari Zifananazo

Back to top button