TRA yataka somo la kodi mitaala ya elimu

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), wamekutana na kamati ya Kitaifa ya uboreshaji wa Mitaala inayoongozwa na Prof.Makenya Maboko jijini Dodoma kwa lengo la kutoa maoni na mapendekezo kuhusu uboreshaji wa mitaala unaondelea.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi TRA, Richard Kayombo, amewasilisha mada ya umuhimu wa kuingiza masuala juu ya elimu ya kodi katika mitaala ya elimu ngazi ya msingi na sekondari.
“TRA inaamini kwamba kama kungekua na somo la kodi linalosomwa na wanafunzi wote katika shule za msingi na sekondari tungeweza kuwa na raia wanaoelewa kodi,” amesema Kayombo.
Amesema, TRA inakusanya kodi kutoka kwa walipa kodi ambao hawana ufahamu na hawajui umuhimu wa kulipa kodi, hivyo kama wanafunzi watafundishwa somo la kodi shuleni, itasaidia kupata raia wenye uelewa mpana kuhusu kodi na kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa hiyari.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati Prof.Maboko, amewashukuru TRA kwa maoni na mapendekezo waliyoyatoa na kuahidi kuyafanyia kazi katika maboresho ya mtaala wa elimu nchini yanayoendelea.