SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limesema kukamilika kwa ukarabati wa Kituo cha Stesheni ya Mvave iliyopo karibu na mbuga ya Saadani mkoani Pwani, itakuwa kichocheo kikubwa cha utalii wa ndani kwa wananchi na wageni wanaotumia usafiri wa reli.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo mwishoni mwa wiki, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara TRC, Never Diamond alisema ushirikiano baina ya shirika hilo na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) unalenga kuangalia miundombinu wezeshi ya kibiashara kati yao ili kujua jinsi ya kukuza utalii wa ndani kupitia usafiri wa reli.
Diamond alisema stesheni ya Mvave ni muhimu katika kukuza utalii, hivyo TRC na TANAPA imeweka mikakati mbalimbali ambayo itawezesha wananchi kutumia muda wao kwenda kupumzika na kuona vivutio vilivyopo nchini.
“TRC inaunga juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza utalii wa ndani na treni ni zaidi ya usafiri kwani ni nafuu salama na unachochea utalii,” alisema.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi kutoka Hifadhi ya Taifa Saadani, Ephraim Mbomo alisema kituo cha Mvave kitabadilisha uwezo wa kupokea wageni wanaotumia magari ya kukodisha na kupata huduma ya moja kwa moja kwa kutumia usafiri wa treni.
“Treni ni usafiri wa uhakika katika vipindi vyote vya masika na kiangazi kwa sababu wakati wa masika magari hupata shida kutokana na miundombinu ya barabara. Hifadhi ya Saadani ni hifadhi pekee ambayo mbuga imekutana na bahari,” alisema.
Alieleza kuwa kwa mwaka hupokea wageni kwa wastani wa watu 20,000, hivyo kupitia usafiri wa treni wanaamini idadi ya wageni itaongezeka na kwamba wamejipanga kupokea wageni watakaoongezeka.
Kwa upande wake, Ofisa Utalii, Athumani Mbae alisema kuwa Hifadhi ya Taifa ya Saadani ina jumla ya kilometa 1,100 ambayo ina vivutio mbalimbali vya wanyama wakiwemo faru, simba, tembo, twiga, chui, nyati , mamba, viboko , swala na pia kuna aina za ndege wa nchi kavu, baharini pamoja na mto Wami.
“Huduma za utalii zinazopatikana katika hifadhi hii ni pamoja na utalii wa boti ili kuweza kuona viboko na mamba kiurahisi, utalii wa kutumia magari pamoja na kutembea kwa miguu. Pia tuna utalii wa usiku kutokana na wanyama ambao sio rahisi kuonekana mchana pamoja na michezo mbalimbali,” alieleza.