DAR ES SALAAM; MKURUGENZI wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba ameiagiza Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kushirikiana na taasisi za serikali kuelezea miradi kwa umma ikiwamo ya kimkakati.
Makoba aliyasema hayo alipozungumza na uongozi wa TSN katika ofisi za kampuni hiyo Tazara, Dar es Salaam jana.
TSN ni wazalishaji wa magazeti ya HabariLEO, HabariLEO Jumapili, Daily News, Sunday News na Daily News Digital.
“Tusomane, taasisi za serikali tuwe na ushirikiano kwa sababu wote tunajenga nyumba moja hatugombei fito sisi wote ni watoto wa baba na mama mmoja,” alisema Makoba.
Aliongeza, “tumepewa kazi kuandaa mkakati wa namna ya kufanya kazi na kuboresha namna ya kuhabarisha umma.”
Alisema kwa sasa nchi ipo kwenye mwaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa na mwakani utafanyika Uchaguzi Mkuu.
Soma pia:https://habarileo.co.tz/mfahamu-msemaji-mkuu-mpya-wa-serikali/
Pia Dira ya Maendeleo la Taifa ya miaka 25 iliyopita inafika mwisho mwakani ambayo watu wanaendelea kutoa maoni. “Haya ni mambo makubwa yanayokwenda kutokea nchini kwetu na sisi ndio jeshi la kuisemea serikali kwa umma.”
Alisema yote haiwezekani kuyafanikisha kama hakutakuwa na ushirikiano.
Makoba anafanya ziara kutembelea taasisi za serikali ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo zaidi ya wiki tatu zilizopita.