COLOMBO, SRILANKA : WAZIRI wa Nishati wa Sri Lanka, Kumara Jayakody, ameeleza jinsi tukio la tumbili kuingia kwenye kituo cha uzalishaji umeme kusini mwa Colombo lilivyopelekea kukatika kwa umeme kote nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari, Jayakody alisema kwamba tumbili huyo aliguswa na transfoma ya gridi ya umeme, jambo lililosababisha usawa kutoweka kwenye mfumo wa umeme, hivyo kuleta madhara kwa usambazaji wa umeme.
Kukatika kwa umeme kulianza mapema Jumapili, majira ya saa 11:00, na kusababisha makundi mengi ya wananchi kutegemea jenereta kwa muda. SOMA : Uzalishaji umeme bwawa la Nyerere wakaribia
Maafisa wa Serikali wamesema kuwa kurejeshwa kwa umeme kutachukua muda, huku vituo muhimu kama vya matibabu na mitambo ya kusafisha maji vikipatiwa kipaumbele ili kuhakikisha huduma muhimu zinaendelea.
Waziri Jayakody alifafanua kuwa kurejeshwa kwa huduma za umeme kutafanyika kwa hatua, na kwamba ni muhimu kwa huduma muhimu kupewa kipaumbele ili kuepusha madhara makubwa kwa jamii.
Kwa sasa, mamlaka za Sri Lanka zinaendelea na jitihada za kurejesha hali ya kawaida, huku wakitoa wito kwa wananchi kuwa wavumilivu.