‘Tumieni mbegu za karanga, alizeti zilizofanyiwa utafiti’
MKURUGENZI Mtendaji wa Wafanyabiashara wa Mbegu Tanzania (TASTA), Dk Bob Shuma amewataka wakulima kutumia mbegu bora za karanga na alizeti zilizofanyiwa utafiti, ili kuongeza uzalishaji utakaowezesha nchi kuwa na mafuta ya kupikia ya kutosha kuanzia ngazi ya kaya.
Amesema hayo jijini hapa wakati alipotembelea shamba la kuzalisha mbegu za mtama , karanga na alizeti la mtaalam wa kilimo Aithan Chaula lililopo Kijiji cha Zinje, Kata ya Mkonze Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Alisema Chaula ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Shirika la Dodoma Agriculture Seeds Production Association (DASPA), alipata ufadhili kupitia wa CIMMYT Mexico chini ya mradi wa AVISA, ambapo huzalisha mbegu, hutoa mafunzo kwa wakulima ambao hugawiwa mbegu kwa lengo la kwenda kuongeza uzalishaji.
Alisema kuwa tangu uhuru zao la karanga lilikuwa likipewa umuhimu kwenye kaya, kwani lilikuwa likiwezesha kukamua mafuta ambayo yalitumika kwa ajili ya kupikia na wengi wamekuwa wakituimia mafuta hayo kwa miaka mingi.
Alisema kuwa wanaendeleza kilimo cha karanga kwa kutumia mbegu bora kwa kuwawezesha wazalishaji wa mbegu ili kuzalisha mbegu ambazo zitagawiwa kwa wakulima katika maeneo yao.
Alisema kuwa Serikali inafanya jitihada kubwa kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija, sekta binafsi pia inahakikisha wakulima wanajiunga kwenye vikundi na kupatiwa mafunzo ambayo huwzesha kuboresha shughuli zao za kilimo ikiwemo kuwafikishia mbegu bora ambazo zitaongeza uzalishaji.
Alisema kuwa TASTA imekuwa na mkakati wa kuwezesha wazalishaji wa mbegu ambao baada ya kuzalisha watazigawa kwa wakulima, ili kuongeza uzalishaji wa mazao kama mtama, karanga na alizeti.
Alisema kuwa walitembelea mashamba ya wakulima ambao wanatumia mbegu zilizofanyiwa utafiti ikiwemo zile za karanga aina ya Nachi 2015 Nari nut 2015 na Naliendele 2016.
“Tumeridhishwa na kazi kubwa iliyofanyika hapa Zinje mashamba ya mbegu yanaonesha kuwa kitakachokwenda kwa wakulima kitakuwa bora na kitaongeza uzalishaju,”alisema
“Karanga ni zao lenye soko zuri ndani na nje ya nchi, kila moja aone wajibu wa kuendeleza jitihada za serikali katika kuhakikisha kunakuwa na ufanisi mkubwa kwenye uzalishaji,” alisema
Mtendaji wa DASPA, Aithan Chaula alisema kuwa wanazalisha mbegu bora, ili kuhakikisha kunakuwa na uzalishaji mkubwa wa mazao.
Alisema kuwa CIMMYT kupitia mradi wa AVISA wanaweza kuwafikia wakulima mkoani Dodoma ambapo katika wilaya ya Chamwino jumla ya kata nane zimefikiwa na Singida Vijijini kata nane.