Tuwathamini watafiti wa kisayansi -Prof Mkenda

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema watafiti wa kisayansi wanapaswa kuthaminiwa kwani uwepo wao unawezesha msukumo wa masuala mengi ikiwemo afya.

Akizungumza leo Oktoba 14, katika sherehe za mafanikio makubwa ya bingwa, mkufunzi na mtafiti wa tiba ya watoto na afya ya vijana, Profesa Karim Manji, Prof Mkenda amesema mtafiti huyo ameiheshimisha Tanzania katika maeneo mengi ya tafiti zake.

Advertisement

Prof Mkenda amesema kuna haja ya kuwekeza zaidi kwenye sayansi ili Tanzania inufaike na uwepo wa watafiti wengi kwenye sekta mbalimbali.

“Sayansi inaingia kwenye maeneo mengi, kila sehemu inahitaji tafiti, lazima tuwekeze kwenye maeneo sayansi,” amesema Prof Mkenda.

Akizungumzia mafanikio ya Prof. Karim Manji, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Profesa Apolinary Kamuhabwa amesema mtaifiti huyo ni mfano wa kuigwa, hazina kwa taifa na mtafiti mkubwa Muhas ingependa kuendelea naye.

Prof Kamuhambwa amesema mafanikio ya Muhas kuwa chuo cha tatu kinachoongoza kwa kufundisha, tafiti, huduma Kusini mwa Jangwa la Sahara pia yamechangiwa uwepo wa Prof Manji kwenye utekelezaji wa tafiti mbalimbali.

Aidha amemshukuru Prof Mkenda kwa kutoa wazo la sherehe za mafanikio hayo katika taaluma yake pia amemshukuru Mwenyekiti wa Baraza la Chuo (Muhas) Dk Harisson Mwakyembe kwa kutoa mwongozo kufanikisha sherehe hizo.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo (Muhas) Dk Harisson Mwakyembe amesema Prof Manji ameiheshimisha Tanzania na Chuo cha Muhas.

Akizungumzia mafanikio yake Profesa Karim Manji ambaye ni mshindi wa tuzo ya Alumni Award of Merit kutoka Shule ya Afya ya Chuo Kikuu cha Harvard (Harvard T.H. Chan School of Public Health) cha Marekani amesema silaha yake ya kwanza ni utu, ubinadamu na kuheshimu watu.

“Unatakiwa kuwa mstahimilivu na mwenye maono pia, sio lazima kuwa na pesa ili iwe njia rahisi kusikiliza shida zao, mawasiliano muhimu pia,”

Akitoa historia yake, Prof Manjia amesema aliwahi kuwa karani wa kusajili magari kuyaendea mafanikio aliyonayo, lakini aliwahi kukutana na changamoto ya kupooza mguu wa kulia hivyo kulazimika kwenda chuo kwa kutumia fimbo.

Amesema miongoni mwa changamoto ni aliwahi kuuza vitumbua, hata hivyo baadhi ya wanafunzi wenzake walikuwa wakimtania shuleni wakitaka huduma ya bidhaa hiyo kwa kufungua begi lake.

Kwa zaidi ya miaka 30, Profesa Manji amekuwa daktari, mkufunzi na mtumishi katika Hospitali ya Taifa na Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Shirikishi, Muhimbili.