TVLA yatoa elimu kuhusu mifugo Sabasaba

DAR ES SALAAM; WAKALA ya Maabara ya Veterinari Tanzania( TVLA), inatoa elimu kuhusu huduma mbalimbali ilizonazo katika Maonesho ya 48 ya Biashara Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba.

Mtendaji Mkuu wa wakala huo, Dk. Stella Bitanyi amesema katika maonesho hayo TVLA inatoa elimu kuhusu huduma zinazotolewa, ikiwemo umuhimu wa uchanjaji wa mifugo, na utambuzi wa magonjwa ya wanyama.

Vikevile uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo, utafiti wa magonjwa ya wanyama na ushauri kuhusu matumizi sahihi ya dawa za mifugo.

Advertisement

Huduma nyingine inayopatikana bandani hapo ni ya elimu ya udhibiti wa wadudu aina ya mbung’o pamoja na kuwadhibiti wadudu hao ambao hueneza ugonjwa wa nagana.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/samia-nyusi-watembelea-mabanda-sabasaba/

Elimu nyingine inayotolewa ni pamoja na kudhibiti magonjwa yaenezwayo na kupe kama ndigana kali na ndigana baridi kwa kuhakiki ubora wa viuatilifu kwa ajili ya kuogesha wanyama, ili kudhibiti kupe.

“Tunaendelea kuwakaribisha wananchi wote waliopo ndani ya viwanja vya maonyesho ya Sabasaba na maeneo mengine, kutembelea banda letu la TVLA lililopo kwenye banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ili kupata elimu kuhusiana na udhibiti wa magojwa ya wanyama, chanjo za mifugo zinazozalishwa na TVLA, ufugaji pamoja na uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo.” amesema.

Wadau mbalimbali waliotembelea banda hilo, wamefurahishwa na elimu inayotolewa hususan uchunguzi wa magonjwa ya mifugo kabla ya kuwatibu pamoja na elimu ya uchanjaji wa mifugo kwani walikuwa wanachanja mifugo yao bila kuipima, kitu ambacho kilikuwa kinasabasha vifo kwa mifugo.