Sportpesa yaipa nguvu Twiga Kings mashindano Afrika Kusini

DAR ES SALAAM: Timu ya taifa ya rugby ya wanaume, Twiga Kings, inatarajia kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Obaro 7s yatakayofanyika Pretoria, Afrika Kusini, Oktoba 24 na 25, 2026, kwa msaada wa kampuni ya SportPesa Tanzania.

Ushiriki huo ni sehemu ya ushirikiano kati ya SportPesa na Chama cha Rugby Tanzania (TRU) unaolenga kuendeleza mchezo huo nchini, kukuza vipaji na kuwapa wachezaji fursa ya kupata uzoefu wa mashindano ya kimataifa.

SportPesa ni mdhamini mkuu wa mashindano ya kitaifa ya SportPesa National Saba Circuit 2026, yanayolenga kuimarisha ushindani, kukuza vipaji na kuongeza ushiriki wa mashabiki wa rugby.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Afisa Mwandamizi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Charles Maguzu, alisema ushiriki wa Twiga Kings katika mashindano ya kimataifa ni fursa muhimu kwa maendeleo ya michezo nchini.

Alisema maendeleo ya michezo yanahitaji uwekezaji katika vipaji, kuimarisha taasisi za michezo na kujenga ushirikiano unaotengeneza fursa endelevu kwa wanamichezo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TRU, Erick Mulamula, alisema maandalizi ya Twiga Kings yamejikita katika kuchagua wachezaji wenye uwezo, kuimarisha mbinu za mchezo na kujenga ushirikiano miongoni mwao.

Alisema kikosi cha mwisho cha wachezaji 13 kilichaguliwa baada ya benchi la ufundi kutathmini uwezo wao uwanjani na utayari wa kushindana katika ngazi ya kimataifa.

Naye mwakilishi wa SportPesa Tanzania, Idrissa Kimaro, alisema kampuni hiyo inaamini uwekezaji katika michezo unapaswa kuwawezesha wanamichezo kukuza vipaji vyao, kupata uzoefu na kufikia viwango vya juu zaidi.

Alisema kupitia ushirikiano na TRU, SportPesa inaunga mkono maendeleo ya rugby kupitia mashindano ya SportPesa National Saba Circuit 2026 na ushiriki wa Twiga Kings katika Obaro 7s.

Kocha Mkuu wa Twiga Kings, Paivin Rugambwa, alisema timu imejiandaa kukabiliana na ushindani wa mashindano hayo, ikilenga kuonyesha uwezo wa wachezaji na kuiwakilisha Tanzania kwa heshima.

Alisema timu hiyo inatarajia kutumia fursa hiyo kujifunza, kupata uzoefu wa kimataifa na kuboresha kiwango chake.

Ushirikiano wa SportPesa na TRU ni sehemu ya kampeni ya miezi mitano inayolenga kuendeleza SportPesa National Saba Circuit 2026 kupitia shughuli za kuongeza mwonekano wa mashindano, kuwashirikisha mashabiki na kutengeneza maudhui ya kidijitali.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button