DAR ES SALAAM: SERIKALI kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Ifakara Health Institute wameweka mkakati wa kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya muda (njiti) kwa kuwawezesha watoa huduma kufanya kazi kwenye mazingira wezeshi.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam katika mkutano wa pili wa Kisayansi wa Afya ya Uzazi wa Mama na Mtoto Mkurugenzi Mkuu wa Ifakara Health Institute Dk Honorati Masanja amesema kitaifa wamepiga hatua kwenye kupunguza vifo vya mama ila watoto bado ni changamoto.
Amesema kazi ya taasisi hiyo ni kufanya tafiti ambazo zitaleta afua mbalimbali za kuboresha Afya ya mama na mtoto.
Aidha amesema changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni upungufu wa wahudumu wa afya hususani kwenye eneo la mama na mtoto hivyo jitihada za makusudi zinahitajika katika kuongeza wahudumu wa afya.
Kwa upande wake Daktari wa watoto kutoka chuo Cha MUHAS Dkt Nahya Salim amesema Tanzania inampango wa kushusha vifo vya watoto wachanga angalau mpaka 15 kwa vizazi hai 1000 ifikapo 2025.
Amesema bado wapo nyuma hivyo kasi kubwa inahitajika mara mbili zaidi au tatu ili kuweza kushusha kasi ya vifo vya watoto wachanga kwani ripoti iliyotolewa na wizara ya Afya vifo vya watoto bado hairidhishi ambapo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita wamepunguza wa asilimia moja tu.
“Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Oktoba 28 mwaka huu na wizara ya Afya Asilimia 1 bado ndogo sana ina maana vifo 24 kutoka vizazi hai 1000 mpaka kwenda 15 hadi kufikia 2025 inabidi kasi zaidi iongezeke,”mesema Dk Nahya.
Amesema Tanzania imetekeleza mpango huu wa kupunguza vifo vya watoto njiti kwa hospitali tano za Dar es Salaam ambazo ni hospital ya Mwananyamala,Temeke Amana na hospitali za mkoa ni Muhimbili pamoja na Mloganzila.
Naye Daktari wa watoto wachanga Dk Rehema Malande amesema vifo vya watoto wachanga ni vingi vikisababishwa na watoto wanaozaliwa chini ya wakati kukabiliwa na changamoto ya upumuaji ambapo serikali imejitahidi kuwekeza vifaa tiba vya kupata hewa ya oxygen.
Hata hivyo amesema changamoto nyingine ni maambukizi ya bacteria kwa watoto wachanga ambapo kwa sasa majengo ya hospital yameboreshwa wafanyakazi wanafanyakazi kwa utulivu.