ILI kuhakikisha Watanzania wanajikwamua kiuchumi, serikali inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu mbalimbali ya kutolea huduma ikiwemo bandari.
Katika kuboresha miundombinu ya bandari serikali imeendelea pia kufanya uboreshaji katika Bandari ya Mtwara kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA).
Uboreshaji huo unahusisha mradi wa ujenzi wa gati jipya uliyogharimu zaidi ya Sh bilioni 157.8 na kutoa fursa nyingi za ajira rasmi na zisizokuwa rasmi kwa wananchi kutoka ndani na nje ya Mtwara hususani katika kipindi cha msimu korosho.
Pia, bandari hiyo imegeuka kivutio kutokana na kuingia kwa meli nyingi za kigeni zinazoingiza na kuchukua shehena za bidhaa mbalimbali ikiwemo korosho kwenda katika masoko ya kimataifa na kuongeza tija ya kilimo cha zao hilo na kuwapa mafanikio wakulima wa zao hilo.
Uboreshaji huo umewezesha TPA kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kutaka korosho zote zinazozalishwa katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma zisafirishwe kupitia bandari hiyo.
Katika mahojiano na gazeti la HabariLEO hivi karibuni wananchi mkoani humo wameelezea namna ambavyo
wananufaika na bandari hiyo kwa kupata ajira hasa kipindi cha msimu wa korosho.
Mkazi wa Mtaa wa Mtepwezi Manispaa ya Mtwara Mikindani, Asia Juma anayefanya shughuli za mamalishe na uuzaji wa vinywaji katika eneo hilo la bandari anampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuagiza korosho ziwe zinasafirishwa kupita bandari ya Mtwara kwa sababu wengi wao wanajipatia kipato kwa shughuli mbalimbali za ujasiriamali kwenye eneo hilo.
“Kusafirishwa kwa korosho kupitia bandari ya Mtwara kumetuongezea fursa ya ajira mfano kuuza chakula, vinywaji mbalimbali na kwa siku mtu mmoja anaweza kupata takribani Sh 30,000 kima cha chini ila misimu iliyopita mfano
2023/2024 ilikuwa hata Sh 20,000 kwa siku haifiki,” anasema Asia.
Mkazi wa Chikongola, Ramadhani Kaseko kutoka Kitongoji cha Luhumbo mkoani Shinyanga anayejishughulisha na shughuli ya mbalimbali bandarini hapo ikiwemo kubeba mizigo, anasema msimu wa mwaka 2024/2025 umekuwa na faida kubwa kwake kwa sababu ameweza kumiliki usafiri aina ya pikipiki kupitia kazi hiyo.
“Mimi kazi yangu ni mchukuzi, msimu huu ni mzuri ikilinganishwa na huko nyuma, binafasi baada ya siku mbili tatu napata takribani Sh 30,000 na hii inategemea na wewe mwenyewe jitihada zako za kufanya kazi, msimu wa mwaka juzi 2023/2024 kipato kilikuwa hakieleweki ndani ya siku mbili tatu tukipata Sh 20,000 inategemea na wingi wa kazi,” anasema Kaseko.
“Msimu huu korosho ni nyingi kwa hiyo na sisi wananchi tunashukuru kazi hapa bandarini zimekuwa nyingi, tunafanya kazi bila kuchoka na mapato tunapata kwa kweli tunashukuru sana serikali yetu,” anasema.
Mkazi wa Mtaa wa Kisutu, Saidi Kilazi ameiomba serikali endelee kutumia bandari ya Mtwara kusafirisha korosho kwani hiyo ni fursa kwao ya kujikwamua kiuchumi na kuweza kuendesha maisha yao kwa uhakika.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Francis Alfred ameishukuru serikali kwa jitihada zake ikiwa ni pamoja na kutoa ruzuku ya pembejeo kwa asilimia 100 na kusababisha ongezeko la uzalishaji huo mkubwa lakini pia uboreshaji wa masoko ya bidhaa za kilimo na matumizi mfumo wa kidijiti wa TMX kwani umesaidia kuongeza ufanisi na ushindani katika biashara ya korosho.
Meneja wa Bandari ya Mtwara, Ferdinand Nyathi anasema katika msimu huo shughuli mbalimbali zinaendelea vizuri bandarini hapo na wananchi wanaendelea na majukumu yao kama kawaida.
Aidha, anasema kwa msimu wa korosho mwaka 2023/2024 Bandari ya Mtwara ilisafirisha takribani tani 253,000 za korosho ghafi na kuongeza kuwa msimu wa mwaka 2024/2025 inatarajia kusafirisha takribani tani 500,000 kwa mujibu wa CBT.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patric Sawala amepongeza uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali Awamu ya Sita katika Bandari ya Mtwara kwani huduma za shehena zimeongezeka bandarini hapo kupitia bidhaa mbambali
ikiwemo zao la korosho.
Waziri wa Uchukuzi Makame Mbarawa alipotembelea bandari hiyo alisema serikali itaendelea kupeleka vitendea kazi katika bandari hiyo ili kuhakikisha ufanisi unaongezeka.
“Napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya kusimamia shughuli mbalimbali za maendeleo kwenye nchi yetu hasa kwetu sisi wa bandari, amekuwa akitupa msukumo mkubwa kuhusu usimamizi wa sekta ya bandari hapa nchini kuanzia usimamizi wenyewe na ujenzi wa miundombinu,” anasema Mbarawa.