Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) limetangaza matokeo ya upimaji wa kitaifa wa Darasa la Nne na Kidato cha Pili kwa watahiniwa wa mwaka 2022, huku ufaulu ukishuka kwa asilimia kadhaa kulinganishwa na mwaka uliopita.
Akizungumza mapema leo Januari 4, 2023 wakati akitangaza matokeo hayo, Katibu Mtendaji wa NECTA, Athumani Amasi amesema ufaulu umeshuka ikilinganishwa na mwaka 2021 ambapo darasa la nne ufaulu ni asilimia 82.95 ikilinganishwa na asilimia 86.30 mwaka 2021.
Amasi amesema kwa upande wa kidato cha pili ufaulu ni asilimia 85.18 ikilinganishwa na mwaka 2021 ambapo ufaulu ulikuwa asilimia 92.32.
KUANGALIA MATOKEO YA DARASA LA NNE BONYEZA HAPA>>>>https://matokeo.necta.go.tz/psle2022rep/psle.htm
Baraza hilo limezuia matokeo ya wanafunzi 442 wa darasa la nne na wanafunzi 258 wa kidato cha pili waliopata matatizo na kushindwa kukamilisha mtihani wa upimaji wa kitaifa.
Aidha limezuia matokeo ya wanafunzi 213 wa darasa la nne na wanafunzi 52 wa kidato cha pili ambao walibainika kufanya udanganyifu na kuvifungia vituo viwili kati ya vituo 18,645 vya mitihani vilivyothibitika kupanga na kufanya udanganyifu.
KUANGALIA MATOKEO YA KIDATO CHA PILI BONYEZA HAPA>>>> https://matokeo.necta.go.tz/ftna2022/ftna.htm
NECTA imesema wanafunzi 2,095 kati ya 2,180 waliofanya mtihani wa marudio wa darasa la saba uliofanyika kati ya Desemba 21 na 22 mwaka 2022 wamefaulu daraja A hadi C sawa na asilimia 96.1.
Wanafunzi hao kati ya 2,194 waliofutiwa matokeo ya mtihani huo na Necta baada ya kubainika kufanya vitendo vya udanganyifu uliofanyika Oktoba 5, 6 mwaka 2022.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athumani Amasi amesema kati ya wanafunzi 2,194 waliofutiwa matokeo waliofanya mtihani 2,180, wachache hawakushiriki mchakato huo kwa sababu mbalimbali, akisema huenda wengine walikwenda nje ya nchi.
Mitihani wa kitaifa wa darasa la nne na kidato cha pili uliofanyika Oct/November 2022 ambapo kwa upande wa darasa la nne Wanafunzi 1,320,700 kati ya 1,592,235 wenye matokeo sawa na 82.95% wamefaulu.