‘Uhuru wa kujieleza, demokrasia vifuate sheria, haki’

UHURU wa kujieleza, uhuru wa kutoa mawazo, uhuru wa demokrasia  na uhuru wa kutoa habari, vyote vinapaswa kutolewa katika misingi yenye kufuata sheria na haki, ili kusiwepo na uvunjifu wa amani.

Hayo yamesemwa leo na Rais Mahakama ya Afrika, inayoshughulika na haki za binadamu, Jaji Imam Aboud, katika mafunzo ya wiki moja ya Majaji wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), jijini Arusha, mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Alisema vyote vikifuatwa haoni kama kutakuwepo na uvunjifu wa amani katika nchi za Afrika na kusisitiza kila mmoja kukumbuka wajibu wake wenye lengo la kulinda amani ya nchi husika.

Rais alitoa wito wa kulindwa kwa uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu, akisema bado haki hizo zinavunjwa na kuuweka mashakani uhuru wa demokrasia katika nchi nyingi Afrika.

Alisema uhuru wa vyombo vya habari na usalama wao ni jambo muhimu, linaloheshimu misingi ya utawala wa kisheria na demokrasia, hivyo majaji wana wajibu wa kuhakikisha wanahabari wanakuwa na uhuru wa kupewa habari  na usalama wao katika nchi za Afrika.

Alisisitiza kwa wanahabari kuhakikisha wanafuata misingi ya uandishi wa habari zinazoeleza uhalisia na ukweli wa jambo, ili kuepuka kuleta mfarakano na machafuko ya ndani ama nchi kwa nchi.

“Mahakama za nchi katika Umoja wa Afrika, zinaweza kushirikiana  na vyombo vya  habari kutoa habari zinazohamasisha amani kuliko habari zenye kuleta mtafaruku, ” alisema.

Naye Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EALA), Jaji Nestory Kayobera, alisema kesi zote zilizopelekwa katika mahakama hiyo, zimetolewa maamuzi, ila suala la utekelezaji wa maamuzi ya mahakama, hilo sio jukumu lako kwani ni jukumu la aliyeleta kesi katika mahakama hiyo.

Alisema katika mahakama hiyo mtu yoyote anaruhusiwa kufungua shauri bila gharama yoyote na kwamba hadi sasa, mahakama hiyo ina mashauri zaidi ya 170, jambo ambalo halijawahi kutokea katika mahakama yoyote ya kimataifa.

Naye Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, David Ngunyale,  alisema mafunzo yanahusu utoaji wa habari, utawala wa sheria na matumizi ya akili bandia  yana lengo la kujua uhuru wenye kufuata sharia, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kijieleza wenye kufuata sheria na sio vinginevyo.

Habari Zifananazo

Back to top button