Ujenzi viwanja vya ndege kuongeza kasi ya uchumi

SERIKALI imesaini mkataba wa Sh bilioni 165 kujenga Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato mkoani Dodoma.

Ujenzi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa kampuni za Sinohydro Corporation limited, M/s Beijing Sino-Aero Construction Engineering Co. limited na M/s China Jiangxi International Economic and Technical Cooperation Co. Ltd za nchini China.

Kiwanja cha Ndege cha Msalato kinatarajiwa kujengwa kwa miezi 36 sanjari na viwanja vingine kwenye mikoa mingine.

Advertisement

Utekelezaji wa miradi hiyo ni maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ukurasa wake wa 90 na 91 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2021/22 – 2025/26) unaobainisha katika ukurasa wake wa 31 kuwa ununuzi wa ndege mpya unaenda pamoja na ujenzi, ukarabati na upanuzi wa viwanja vya ndege vya mikoa na vya kimataifa.

Katika ukurasa wa 274 ilani hiyo inaelekeza kuanza ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Msalato kwa ajili ya kuboresha usafiri wa anga katika Jiji la Dodoma.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameagiza kiwanja cha ndege Msalato kijengwe kwa kuzingatia viwango vilivyokubaliwa kimkataba na kwa kuzingatia muda uliopangwa.

“Serikali tumejipanga kuhakikisha malipo kwa mkandarasi yanalipwa kwa wakati, hivyo hakikisheni Mkandarasi anatekeleza majukumu yake yote kwa mujibu wa mkataba, hatutakubali visingizio vyovyote”alisema Profesa Mbarawa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Joseph Malongo alisema wamejipanga kukamilisha taratibu za kiutendaji zilizobaki kwa wakati.

“Mkataba umekamilika tunawataka wakandarasi na wasimamizi waende site mara moja, wizara tuko tayari kwa kazi,’ alisema Malongo.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Babaraba Tanzania (Tanroads), Rogatus Mativila alisema ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Msalato utahusisha awamu mbili ukiwemo ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege na ujenzi wa majengo likiwemo la abiria.

Kiwanja hicho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka.

Hivi karibuni Profesa Mbarawa alisema bungeni kuwa Sh milioni 86,102.522 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya ndege saba na ukarabati wa vingine vitatu katika mwaka wa huu wa fedha 2022/2023.

Aliwaeleza wabunge kuwa kati ya fedha hizo, Sh milioni 54,955.206 ni fedha za ndani na Sh milioni 31,147.316 ni fedha za nje.

Miongoni mwa viwanja vya ndege vitakavyojengwa kupitia fedha hizo ni kiwanja cha ndege cha Kigoma na akasema mradi huo umetengewa Sh milioni 7,630.90.

Profesa Mbarawa alisema ujenzi huo utahusu ujenzi wa jengo la abiria na miundombinu yake ukiwemo ukarabati na upanuzi wa maegesho ya ndege, maegesho ya magari na barabara ya kuingia na kutoka kiwanjani.

Pia itahusu usimikaji wa taa na mitambo ya kuongozea ndege, ujenzi wa uzio wa usalama, jengo la kuongozea ndege na jengo la uchunguzi wa hali ya hewa.

Profesa Mbarawa alisema fedha hizo pia zitatumika kujenga wa kiwanja cha ndege cha Mpanda kilichotengewa Sh milioni 12.10 kwa ajili ya maandalizi ya usanifu wa jengo la abiria.

Viwanja vingine vitakavyojengwa ni kiwanja cha ndege cha Tabora kilichotengwa Sh milioni 3,695.32, ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Songwe kilichotengewa Sh milioni 10,106.46,na  ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Sumbawanga kilichotengewa Sh milioni 3,692.90.

Profesa Mbara alisema ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Shinyanga umetengewa Sh milioni 3,692.90, ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Bukoba Sh milioni 12.10 na ujenzi wa jengo la tatu la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Sh milioni 54.346.

Alisema kazi nyingine zitakazofanyika katika mwaka huu wa fedha ni ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Mwanza kwa gharama ya Sh milioni 5,300.48, ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Arusha kilichotengewa Sh milioni 242.02 na ukarabati wa Kiwanja cha ndege cha Mtwara kilichotengewa Sh milioni 4,947.79.

 

 

/* */