Ulevi wa kupindukia watajwa kuwa tatizo la afya ya akili

Sababu wanaume kuongoza magonjwa ya akili zatajwa

ULEVI wa kupindukia, suala la mahusiano ama kushindwa kumaliza masomo kwa wakati ni miongoni mwa changamoto inayosababisha tatizo la afya ya akili kwa wafanyakazi pamoja na wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Hayo yalielezwa na Mkurugenzi wa Huduma za Jamii katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Mwajuma Vuzo wakati wa maadhimisho ya siku ya afya ya akili yaliyoadhimishwa na chuo hicho.

Dk Vuzo alisema mambo hayo yanaikumba jumuiya ya chuo hicho kutokana na changamoto mbalimbali mhusika anazopitia hali inayomfanya awe na tatizo la afya ya akili.

Advertisement

Alisema jambo hilo wanapolibaini kitengo cha ushauri na unasihi chuoni hapo kinawaelekeza wafanyakazi wenye changamoto hiyo kwa usiri wafike na kupata huduma za ushauri nasaha ambapo kuna wataalamu kutoka ndani na nje ya chuo ili waweze kuwasaidia.

Alisema utekelezaji wa sera ya ushauri na unasihi umekuwa na ufanisi mkubwa kutokana na muundo wa kitengo cha ushauri na unasihi na namna ambavyo kitengo kinafanya kazi na vitengo mbalimbali vya chuo.

“Kwa ujumla wafanyakazi ni wachache wanaohudumiwa na kitengo, nawashauri wafanyakazi wote wasisite kupata huduma kwenye kitengo ili kutatua changamoto zao mbalimbali,” alisema.

Alisema suala hilo limekuwa likionekana ni geni japokuwa elimu yake hutolewa mara kwa mara hivyo endapo mfanyakazi ana changamoto ni muhimu kupata huduma hiyo.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Unasihi, Dk Bernadetha Rushahu wa UDSM alisema wamewafikia wafanyakazi na wanafunzi wengi katika uelimishaji na uhitaji wa huduma ya ushauri na unasihi kwa jumuiya nzima ya UDSM.

Alisema elimu hiyo imesaidia kutambua uwepo wa huduma ya ushauri na unasihi kwa wanajumuiya wa chuo hicho ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakumba katika maisha yao ya kila siku.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa chuo, Profesa William Anangisye alisema kuwa siku ya afya ya akili huadhimishwa kimataifa kwa kuangalia unyeti na upana wa suala hilo.

Alisema afya ya akili ni suala ambalo jumuiya ya kimataifa imeona ipewe uzito unaotakiwa.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *