WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu, amekabidhi magari matano kwa ajili ya kampeni ya kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika halmashauri tano za Mkoa wa Kagera, huku akisema Kagera ipo salama na yeyote anayetaka kuja na aje bila hofu.
“Kagera ni salama, atakaye na aje, jitihada kubwa tunazozifanya ni kuchukua tu tahadhari, wasiwasi ndio akili, mpaka sasa nchi yetu hatuna mgonjwa yeyote, tupo salama…….
‘Watanzania wasiwe na hofu, wiki ijayo kuna kilele cha Mwenge hapa Bukoba, watu wasiogope kuja, tupo salama mpaka sasa,” amesema Ummy na kuongeza:
“Hata hivyo, tunawaomba viongozi wa dini zote, na kila Mtanzania kwa imani yake tuombe Mungu atuvushe ugonjwa huu usiingie nchi mwetu,” amesema.
Halmashauri zilizopatiwa magari ya kampeni ni zile zilizopo kwenye hatari kubwa ya kupata mlipuko wa ugonjwa wa Ebola kutokana na kupakana kwa karibu na Uganda ambazo ni Kyerwa, Misenyi, Karagwe, Muleba na Ngara.
Pia Ummy amekabidhi vizibao kwa madereva bodaboda 35 wa Halmashauri ya Bukoba mjini, vipeperushi na ‘flashi’ yenye ujumbe wa namna ya kujikinga na ugonjwa wa Ebola na kutoa taarifa za wahisiwa wa ugonjwa.
Akizungumza wilayani Bukoba leo Oktoba 6, 2022, Ummy amesema lengo ni kuwafikia bodaboda 100 kila Halmashauri na Bodaboda hao ndio mabalozi wa kudhibiti Ebola
“Bodaboda nyie ndio mabalozi wetu, ukimbeba abiria akimuona anakohoa tu toa taarifa, umemuona anatapika au ana dalili ya homa mripoti haraka ulipomshusha, ili afuatiliwe, namba ya kutoa taarifa ni 199 namba hii ni bure, na watoa huduma wetu watafanya kazi saa 24,” amesema.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma, Dk Amma Kasangala, amesema kampeni hiyo ni ya nyumba kwa nyumba na itafanyika kwa muda wa mwezi mmoja.
“Madereva wa daladala, bajaji, pikipiki tumewapa vipeperushi na flashi video ambavyo kila abiria atakayetumia usafiri mmojawapo basi atakutana na ujumbe wa kudhibiti Ebola,” amesema na kuongeza kuwa magari maalum ya matangazo yataendelea kupita mitaani kuhamasisha na kutoa elimu ya kujikinga.