United, Palace zapigwa faini
MANCHESTER United na Crystal Palace zimepigwa faini ya pauni 55,000 na chama cha soka nchini England FA kwa kushindwa kuzuia wachezaji wao ambao waliingia kwenye vurugu katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa Februari 12, 2023.
Katika mchezo huo kiungo wa United Carlos Casemiro alioneshwa kadi nyekundu baada ya kumkaba shingoni kiungo wa Palace Will Hughes wakati vurugu hizo zikiendelea.
Vurugu hizo zilianza kwa kiungo wa Palace Jeffrey Schlupp kumfanyia madhambi winga wa United Antony na wote wawili wakapewa kadi ya njano. United wamekubali shtaka hilo huku Palace wakikanusha.
Msemaji wa Chama cha Soka alisema: “Manchester United na Crystal Palace walikubali na kukana kwamba walishindwa kuhakikisha wachezaji wao wanajiendesha kwa utaratibu na kujiepusha na uvunjifu wa sheria na kanuni za soka.
“Tume huru ya udhibiti baadaye ilipata mashtaka dhidi ya Crystal Palace kuthibitishwa na kuzitoza faini za vilabu vyote viwili.” Alisema.