‘Upo utaratibu kutambua walio sekta isiyo rasmi’

DODOMA; MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA), ina utaratibu wa kutambua walipa kodi kulingana na mitaa. Bunge limeelezwa.
Naibu Waziri wa Fedha Hamad Hassan Chande, ametoa kauli hiyo bungeni leo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Neema Lugangira aliyetaka kujua hatua ambayo serikali imepiga katika kurasimisha biashara za sekta isiyo rasmi ili kuongeza uchumi wa nchi.
“Serikali kupitia TRA ina utaratibu wa kuwatambua walipakodi kulingana na mitaa (Blocks Management System) ambayo husimamiwa na maofisa kodi ambao hutembelea mitaa husika na kufanya ukaguzi kwa wafanyabiashara ili kujua mwenendo wao katika kulipa kodi.
“Vilevile Serikali kupitia TRA imeendelea kuwatambua na kuwasajili wafanyabiashara wadogo wadogo pamoja na kuwapa elimu juu ya huduma za kikodi ikiwa ni pamoja na TIN.
“Sambamba na hilo, Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, TRA, TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maendeleo na Makazi, na Mifuko ya Kijamii na Wizara ya Viwanda, ipo katika zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya kijiditali kwa wafanyabiashara ndogondogo kwa lengo la kuwatambua, kuwawezesha kimitaji na kufuatilia kwa karibu maendeleo ya biashara zao.
“Lengo la Mkakati huu ni kuwakuza wafanyabiashara na hatimaye kuwaingiza kwenye mfumo rasmi ambao wataweza kusajiliwa na kulipa kodi,” amesema Naibu Waziri.