MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Geita (GEUWASA) imeweka wazi, mpaka sasa hali ya usambazaji na upatikanaji wa maji kwenye maeneo ya mijini ndani ya mkoa wa Geita imefikia asilimia 75.
Maeneo hayo ya mijini yanayohudumiwa na Geuwasa yanagusa Manispaa ya Geita yenye kata 13, kata sita za wilaya ya Mbogwe pamoja na kata nane za Mamlaka ya mji mdogo wa Katoro.
Mkurugenzi wa Geuwasa, Mhandisi Franki Changawa amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya upatikanaji wa maji kwenye kikao cha Kamati ya Kamisheni ya mkoa wa Geita.
Mhandisi Changawa amesema mpaka sasa kuna vituo 122 vya kuchotea maji kwenye maeneo yote huku kukiwa na matenki ya maji yenye uwezo wa kuhifahi lita milioni 3.845.
“Mtandao wa mabomba ya maji tumesambaza kilomita 507.28 inayojumuisha kilomita 303 mjini Geita, Kilomita 98.45 zipo Mbogwe na Katoro tumelaza mabomba kilomita 106”, ameeleza.
Aidha ametaja miradi mbalimbali inayoendelea ikiwemo mradi wa maji Bung’wangoko, pamoja na mradi wa upanuzi wa mtambo wa kutibu maji Nyankanga uliofikia asilimia 97.
“Tuna mradi wa maji wa miji 28 ambapo kwa wilaya ya Geita umefikia asilimia 37 ukitekelezwa kwa thamani ya dola za kimarekani milioni 57” amesema Changawa.
Amesema mradi wa miji 28 una matenki matano kati yake matenki manne yameshakamilika ikiwemo tenki la lita laki mbili eneo ya Senga na lita laki saba eneo la Kaseni.
Ameongeza pia eneo la Kagu kuna tenki la lita milioni moja, Mpomvu kuna tenki la lita milioni mbili huku tenki mojakubwa la lita milioni tano linatarajiwa kukamilika Februari 2025.
“Katika hali ya uondoshaji wa maji taka kuna mitambo ambayo ipo pale yenye uwezo wa kuondosha lita laki tano kwa siku,” amesema Changawa.