Ushirikiano Tanzania, Japan mfano ukuaji uwekezaji kimataifa

USHIRIKIANO baina ya Tanzania na Japan unaelezwa kuzidi kukua na kuimarika hasa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kidiplomasia.

Kwa mfano mauzo ya biashara kati ya nchi hizo mbili yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni saba mwaka 2023 hadi Dola bilioni 37 kwa mwaka 2024.

Kasi ya ukuaji huu inaashiria wazi kuwa ushirikiano baina ya nchi hizo ni mkubwa na wa kimkakati unaolenga kuleta mapinduzi ya kiuchumi hasa kwa Tanzania ambayo bado inajipanga kukua kiuchumi zaidi ya Japan iliyofika mbali.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya Siku ya Tanzania kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Osaka (World Expo Osaka 2025) nchini Japan, alisema ushirikiano wa Tanzania na Japan unazidi kuota mizizi.

Alisema Wajapan wanapenda sana bidhaa kutoka Tanzania zikiwemo za kilimo kama chai, kahawa, ufuta, tumbaku, tingatinga, vinyago, katani, viungo kama karafuu na madini yanayopatikana nchini.

Hii inamaana bidhaa hizo zina soko kubwa Japan, hivyo ni kazi kwetu kuimarisha ubora na uaminifu wa kuzizalisha kwa viwango vya kimataifa ili tuendelee kushika soko hilo.

Kutokana na ushirikiano huo, Majaliwa aliwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan na duniani kote kuja kuwekeza katika maeneo ya elimu, afya, miundombinu, nishati, kilimo na utalii kwani Tanzania imeweka  mazingira mazuri ya uwekezaji na pia ina amani na utulivu.

Kete hii ya amani na utulivu inapaswa kuwekewa nguvu kuelezwa duniani kote. Ni wazi hakuna mwekezaji atakayewekeza katika nchi yenye vurugu, hivyo amani ya Tanzania ni mtaji mkubwa wa uwekezaji kwa nchi kama Japan na nyingine zilizopiga hatua kubwa kiuchumi.

Ni wazi Tanzania licha ya kuwa na fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo ardhi yenye rutuba, amani na utulivu, pia ni kitovu cha biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Kusini na Kati kwa kuwa inapakana na nchi saba ambazo ni Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Zambia, Malawi na Msumbuji  hivyo wawekezaji wanapata masoko ya uhakika katika mataifa hayo.

Mbali na Japan ambayo tayari ushirikiano wake na Tanzania una tija kubwa, tunajua yapo mataifa mengine makubwa duniani kama Marekani, China, Ufaransa, Ujerumani, India na mengine mengi ambayo ushirikiano na Tanzania ni mkubwa.

Tunaunga mkono wito wa Waziri Mkuu kuwakaribisha wawekezaji nchini kwa kuwa amani, utulivu na mazingira rafiki na mazuri ya uwekezaji ni nyenzo muhimu kuwahakikishia uwekezaji wenye tija.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button