DODOMA: WAKATI wimbi kubwa la vitendo vya ukatili wa kijinsia na ushoga vikiwa vimeshamiri, serikali imetoa msimamo wake kuwa atakayebainika kufanya vitendo hivyo ataadhibiwa miaka 30 jela huku ikiwa imeunda kamati 18,186 za ulinzi na usalama wa wanawake na watoto.
Akizungumza leo Mei 07, 2024 Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis amesema Kamati hizo zinatoa elimu na taarifa ya masuala ya ukatili wa kijinsia, ambapo pia imeunda madawati 2405.
Katika shule za msingi madawati 1765, sekondari madawati 640 madawati ya kijinsia katika vyuo vikuu 256, madawati 115 katika maeneo ya sokoni pamoja na madawati 420 katika vituo vya polisi yanayoshughulikia kesi za ukatili wa kijinsia na kingono.
Isome pia: https://habarileo.co.tz/mikoa-3-vinara-ukatili-wa-kijinsia/
Aidha, akitoa msimamo wa serikali, Mwanaidi amesema kitendo cha kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja ni kosa la jinai kwa kifungu namba 154 cha sheria.
“Pia, kanuni ya adhabu sura ya 16 inatambua mtu yoyote ambaye atapatika na hatia ataadhibiwa kifungo cha miaka 30 ikithibitika na mtendewa aliridhia kufanya kitendo hicho basi nae atahusika na kifungo hicho,” amesema.
Amesema, adhabu hiyo ipo kisheria na kwamba kinachotakiwa ni kufanyiwa marekebisho ya sheria.
Msimamo huo wa serikali umekuja baada ya Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Magharibi Zanzibar, Tauhida Gallos kuhoji mpango wa serikali kudhibiti masuala ya ukatili wa wanawake na watoto.
Aidha, bunge la mwaka 2023 liliishauri serikal kufanya utafiti na kuainisha mapungufu yaliyopo katika Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya mwaka 1998 na kuwasilisha muswada wa marekebisho hayo bungeni ili yaidhinishwe kwa minajili ya kukabiliana na wimbi la mapenzi ya jinsia moja.
Spika wa Bunge la Tanzania Dk Tulia Ackson aliyekuwa akijibu ombi la Mbunge.
Miongoni mwa maboresho yanayotajwa na wabunge ni kuongeza ukali wa adhabu kwa watu watakaobainika kujihusisha na vitendo vya mapenzi ya jinsia moja na kutambua vitendo vya usagaji kama kosa la jinai.
Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kifungu cha 154 kimebainisha adhabu ya Makosa ya kinyume cha maumbile Sheria Na. 47 ya 1954 kifungu cha tatu na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya 1998 kifungu cha 16 kuwa ni kifungo cha miaka 30 jela au kifungo cha maisha.
Isome pia hapa: https://habarileo.co.tz/wazazi-ccm-wataka-vita-dhidi-ya-ushoga-iongezwe/
“Mtu yeyote ambaye anamuingilia mtu yeyote kinyume cha maumbile au, anamuingilia mnyama kimwili au anamruhusu mwanaume kumuingilia yeye mwanaume au mwanamke kinyume cha maumbile, atakuwa ametenda kosa, na atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha maisha na wakati mwingine kifungo kisichopungua miaka thelathini.
Ikiwa kosa limetendwa chini ya kifungu kidogo cha (1) cha kifungu hiki dhidi ya mtoto wa chini ya miaka 10, mkosaji atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha maisha,” inasomeka sehemu ya sheria hiyo.