ZANZIBAR;SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kitendo cha kuongeza ushuru kwa bidhaa za kuku pamoja na samaki wanaotoka nje ya nchi kimelenga kuwaongezea uwezo wafugaji wa ndani kumudu soko la ndani.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Hamza Hassan Juma wakati akitoa ufafanuzi na kujibu hoja za baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochangia bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Alisema kilio cha muda mrefu cha wafugaji wa ndani ni kuwapo kwa bidhaa za kuku wanaotoka nje ya nchi wanaouzwa kwa bei rahisi na hivyo kuangusha soko lao kiasi cha kushindwa kumudu ushindani wa uzalishaji.
Isome pia:https://habarileo.co.tz/mkakati-kuhakikisha-usalama-ubora-vyakula-vya-mifugo/
Juma alisema hicho ni kilio cha muda mrefu kutoka kwa jumuiya ya wafugaji ambacho katika bajeti ya serikali kwa mwaka 2024/2025 serikali imependekeza kuongezea ushuru kwa bidhaa hizo.
Alisema wapo wawekezaji wawili waliojitokeza kutekeleza mradi mkubwa wa ufugaji wa kuku pamoja na Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu kutekeleza miradi ya ufugaji wa mazao ya baharini ikiwamo samaki na matango bahari kwa wajasiriamali.
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis alisema amekutana na jumuiya ya wafugaji Zanzibar ambao wamefurahishwa na uamuzi wa serikali kupendekeza kuongeza ushuru kwa kuku wanaotoka nje ya nchi pamoja na samaki.