WAZIRI wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar, Rahma Kassim Ali, amesema kuwa tabia za uvamizi na uuzaji holela wa maeneo ya ardhi ya akiba imechangia ongezeko la migogoro ya ardhi Zanzibar.
Rahma amesema hayo alipokutana na Masheha wa Wilaya ya Kusini Unguja kwenye kikao maalum kilichofanyika ofisi za Mkuu wa Wilaya hiyo.
Amesema kutokana na tabia hizo, Wizara hiyo itahakikisha inaweka mikakati imara ya udhibiti wa uuzaji ardhi kiholela hasa katika maeneo ya ardhi ya akiba yaliyotengwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Ameongeza kuwa Wilaya ya Kusini Unguja inaongoza kwa uvamizi na uuzaji wa ardhi kiholela hasa katika maeneo ya fukwe za bahari yiliyopo wazi, hivyo kutokana uwezo wa wizara yake kupewa dhamana ya usimamizi wa ardhi kwa mujibu wa tangazo la kisheria Namba 137 ya Mwaka 2020, itahakikisha inayadhibiti maeneo hayo.
“ Wilaya ya Kusini Unguja inaongoza kwa uvamizi na uuzaji wa maeneo kiholela, hasa maeneo ya fukwe na yaliyo wazi, hivyo kwa vile wizara yangu ndio iliyopewa dhamana ya usimamizi wa ardhi kwa mujibu wa sheria, nitahakikisha ninayadhibiti maeneo hayo na atakaebainikia kwenda kinyume hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” amesema.
Amewataka masheha hao kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika usimamizi wa masuala ya ardhi pamoja na kufanya kazi zao ipasavyo, kwa kutojihusiha na vitendo vya uuzaji wa ardhi bila kufuata sheria zilizowekwa.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Mzee Ali Haji amesema kwa mujibu wa Sheria ya ardhi Namba 12 ya mwaka 1992 imekataza kuuziwa ardhi mgeni yeyote bali atatakiwa kukodishwa kwa ajili ya uwekezaji na sio vinginevyo.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mipango Miji na Vijiji Kutoka Kamisheni ya Ardhi Muchi Juma Ameir, amesema tayari Kamisheni ya Ardhi imeyaainisha maeneo yote yenye ardhi ya akiba yaliyoko katika Mkoa wa Kusini Unguja yakiwemo Paje, Muungoni,na Muyuni kwa lengo la kuyapanga na kuyapima kwa kuyawekea alama na kuyadhibiti ili yasiweze kuvamiwa kwa uuzaji wa viwanja kiholea