UVCCM waonywa kubweteka kujitafutia maendeleo

VIONGOZI wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma wametakiwa kutobweteka badala yake wafanye kazi za kujiingizia kipato pamoja na kukisaidia chama kimaendeleo.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti mstaafu wa Jumuiya hiyo, Hassan Kidoke, ambaye amemaliza muda wake alipokuwa akizungumza na vijana wa wilaya kwenye mkutano mkuu wa uchaguzi wa kuwapata viongozi watakaongoza kwa miaka mitano.

Mkutano huo ulifanyika jijini Dodoma na kushirikisha vijana kutoka kata zote za Wilaya ya Bahi, Kidoke amewataka viongozi waliochaguliwa katika nafasi ngazi mbalimbali za Jumuiya hiyo kufanya kazi za kujiingizia kipato pamoja na kukisaidia chama kiendelee kudumu badala ya kulewa na kubweteka na madaraka.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Mnkunda aliwataka vijana waliochaguliwa kukemea maovu yakiwemo vitendo vya rushwa.

Alisema kuwa wamepewa dhamana na vijana wenzao ili waweze kuwatumikia na kuleta mabadiliko ndani ya chama na jumuiya hiyo huku wakikataa kutumika kwenye vitendo vya rushwa katika chaguzi mbalimbali za chama.

Mnkunda ambaye alikuwa msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, pia amewataka vijana hao kuendeleza mema yaliyofanywa na viongozi waliowatangulia.

Pia wametakiwa vijana hao kutotumika na wagombea wa jumuiya zingine kwa kuwafanyia kampeni zinazoashiria kuwepo kwa rushwa, Chama Cha Mapinduzi kinawataka viongozi wenye uadilifu na sifa ya kuongoza.

Katika uchaguzi huo Mwenyekiti aliyechaguliwa ni Justine Sangula huku nafasi mbalimbali za uwakilishi zikiwapata viongozi wake.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button