Uwekezaji mifuko hifadhi ya jamii wafikia tril 14/-

THAMANI ya uwekezaji wa mifuko ya Jamii ilikuwa imefikia jumla ya Shilingi trilioni 14.04, Bunge limefahamishwa leo asubuhi.

Akichanganua kiasi hicho kwa wabunge, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi amesema kati ya Sh trilioni 14.04,  Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umewekeza jumla ya Sh trilioni 6.03 huku Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ukiwa umewekeza umewekeza jumla ya Sh trilioni 7.49.

Akinukuu ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2022, Katambi ameongeza kuwa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umewekeza jumla ya Sh bilioni 521.94.

Katambi alitoa maelezo yake wakati akijibu swali Na. 332 lililoulizwa na Mbunge Halima Mdee aliyetaka kujua tahami ya mifuko hiyo tangu kuanzishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii.

Aidha, Mbunge huyo alitaka kufahamu faida na hasara za uwekezaji wa mifuko hiyo.

Kuhusu faida, Katambi ameliambia Bunge kuwa uwekezaji huu ni kulinda thamani ya michango ya wanachama na kuhakikisha mifuko inakuwa endelevu ili kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulipa mafao.

“Aidha, uwekezaji huu huchangia pia kuongeza ajira, mapato ya Serikali kupitia kodi na kuchochea shughuli za uchumi. Mheshimiwa Spika, kama ilivyo katika uwekezaji wowote kuna vihatarishi (risk) ambavyo vinaweza kusababisha hasara kwa baadhi ya uwekezaji,” amesema.

Katambi ameongeza kuwa hasara zilizojitokeza kwa uwekezaji uliofanywa na mifuko ni pamoja na kutolipwa kwa wakati kwa mikopo iliyotolewa kwa wanufaika mbalimbali na baadhi ya miradi kutofanya vizuri ikilinganishwa na matarajio yaliyokuwepo wakati wa kubuni miradi hiyo.

Hata hivyo, Halima Mdee hakuridhika na majibu ya Naibu Waziri hususani faida na hasara na kuomba mwongozo baada ya kipindi cha Maswali na Majibu lakini alipoteza fursa hiyo baada ya kukosea kanuni ya kuwasilisha hoja yake.

Habari Zifananazo

Back to top button