UWT yaonya wabunge Kigoma

KIGOMA: MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda amewaonya  wabunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma wasiokutana na wananchi kusikiliza kero na wasiotekeleza mipango ya maendeleo kwenye majimbo yao.

Alisema hayo kwenye mkutano wa majumuisho wa ziara ya siku saba mkoani Kigoma ambako alitembelea miradi 98 na kufanya mikutano 90 kati ya hiyo, mikutano 74 ikiwa ni ya hadhara na wananchi.

Amesema serikali ya CCM inafanya kazi kubwa kutekeleza miradi katika majimbo manane mkoani Kigoma na sasa mkoa unapiga hatua ya maendeleo.

Advertisement

SOMA: UWT yataka viongozi wa kuipa ushindi 2024, 2025

Chatanda alisema kati miradi hiyo ipo ya kimkakati ukiwamo ujenzi wa barabara za kiwango cha lami, mradi wa kupeleka umeme wa gridi ya taifa, uimarishaji wa usafiri katika Ziwa Tanganyika, upanuzi wa kiwanja cha ndege, miradi ya maji, afya na elimu.

Amesema kutekelezwa kwa miradi hiyo kunahitaji mchango wa ofisi ya mkuu wa mkoa, wakuu wa wilaya,halmashauri na wabunge wa mkoa huo.

Alipongeza viongozi hao kwa kazi ya kutetea, kusimamia na kuelekeza miradi itekelezwe kwa ufanisi. Chatanda alisema baadhi ya wabunge wamefanya kazi ya kusukuma maendeleo kwenye majimbo yao lakini katika baadhi ya majimbo wabunge wamelalamikiwa kwa kutofanya kazi na kutokuwapo kwenye majimbo kwa muda mrefu.

“Wabunge wanayo maelekezo kutoka kwenye chama kuhusu kufanya mikutano, kusikiliza kero za wananchi na kuibua na kutekeleza miradi ya wananchi ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM,”alisema.

Aliongeza: “Wanaofanya vizuri wanapongezwa lakini wasiofanya kazi majibu watayapa wakati wa mchujo wa kura za maoni, hatuwatishi, muda wao wajirekebishe wasipofanya hivyo panga linawahusu”.

SOMA:https://shinyanga.go.tz/new/ndugu-mary-chatanda-aipongeza-manispaa-ya-shinyanga-kwa-utekelezaji-mzuri-wa-miradi-ya-maendeleo

Chatanda ameonya watendaji wa chama hicho kwenye ngazi za mikoa, wilaya na kata akiwataka waache kuwa wapambe wa wagombea kwa kuwakumbatia na kutembea nao wakati huu ambao taratibu za uchaguzi kwa ajili ya kupata wagombea wa nafasi mbalimbali haujaanza.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba ameipongeza UWT kwa kufanya ziara ambazo zimeenda sambamba na ukaguzi wa miradi na kufanya mikutano hadi kwenye ngazi za vijiji. Katimba alifuatana na Chatanda kwenye majimbo yote ya Mkoa wa Kigoma.