VETA Kigamboni kujengwa kwa Sh bilioni 4.37

KIGAMBONI: Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Wilaya ya Kigamboni unatarajiwa kugharimu jumla ya Sh bilioni 4.37, huku utekelezaji wa mradi huo ukiwa umefikia asilimia 85 na baadhi ya kozi zikitarajiwa kuanza Novemba 2026.


‎
‎Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Mei 26, 2023, kwa mfumo wa nguvu kazi ya ndani (Force Account) kupitia Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Dar es Salaam, chini ya usimamizi wa VETA Makao Makuu.
‎
‎Amesema awamu ya kwanza ya mradi inahusisha ujenzi wa majengo 19 yaliyokadiriwa kugharimu Sh bilioni 3.2, huku awamu ya pili ikihusisha majengo matano yenye gharama ya Sh bilioni 1.17, na kufanya jumla ya majengo kufikia 24.


‎
‎Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Hussein Mohamed Omar, ameridhishwa na hatua iliyofikiwa katika ujenzi huo, akieleza kuwa maendeleo ya madarasa na karakana yanaonesha uwezekano wa baadhi ya kozi kuanza Novemba mwaka huu.


‎
‎Dk. Omar ameleza kuridhishwa kwake baada ya kufanya ziara leo, tarehe 9 Oktoba 2026 katika mradi wa ujenzi wa chuo hicho unaotekelezwa katika eneo la Gezaulole, kata ya Somangila Mtaa wa Kizani, akiwa amembatana na baadhi ya viongozi kutoka Wizara hiyo.


‎
‎
‎Dk. Omar ameitaka VETA kuhakikisha chuo hicho kinawanufaisha kiuchumi wakazi wa Kigamboni, huku akisisitiza viongozi wa Halmashauri, hususan madiwani, kupewa taarifa za mradi ili waweze kuhamasisha vijana kujiunga na mafunzo.


‎
‎Amesema chuo hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 675 wa kozi za muda mrefu na 2,000 wa mafunzo ya muda mfupi, pamoja na bweni lenye uwezo wa kulaza wanafunzi 320, wakiwemo wavulana 160 na wasichana 160.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button