Vijana 260 kujifunza kilimo Israel

SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na Israel wameendelea na jitihada za kukuza ujuzi kwa vijana kwenye sekta ya kilimo, ambapo takribani vijana 260 wanapelekwa nchini Israel kupata mafunzo ya kilimo.

Lengo kubwa la kuwapeleka vijana hao nchini Israel ni pale watakaporudi waweze kujiajiri na kufanikiwa kupata fursa ya kuajiriwa katika sekta ya kilimo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kuwaaga vijana wanaotarajiwa kwenda nchini Israel kuhudhuria mafunzo ya kilimo cha kisasa, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Profesa Jamal Katundu amesema wanafunzi hao watakuwa na mafunzo ya darasani lakini pia mafunzo kwa vitendo.

Amesema fursa hiyo imepatilana kutokana na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu wa Israel ambao wamekuwa wakizungumzia suala hilo kwa ajili ya kujenga uwezo wa vijana kwenye sekta ya kilimo

“Tangu mwaka 2019 tumekuwa tukipeleka vijana wa kitanzania nje ya nchi kwaajili ya kupata mafunzo ya kilimo nchini Israel, wanafunzi hao wanakuwa na mafunzo ya darasani lakini pia mafunzo ya vitendo”

“Serikali chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Kilimo tuna mradi wetu wa BBT, hivyo vijana hawa tuna wa encourage wakirudi wawe walimu kwa ujuzi walioupata waweze kujiajiri kwenye sekta ya kilimo lakini pia waweze kuajiriwa kwa urahisi,”amesema Prof. Katundu

Alisema wanafunzi hao wanapokuwa nchini Israel ni fursa nzuri kwao kwani mbali na kupata mafunzo ya utaalamu wa kisasa, lakini pia wanakua wanafanya kazi na kulipwa.

Prof. Katundu amewasihi vijana hao kuitumia elimu wanayoipata nchini humo, ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuwa chachu katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Naibu Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam anayeshughulikia mambo ya utafiti Prof. Nelson Boniface amesema fursa hizi zinazotolewa na BBT, ambayo ni mafunzo kwa vitendo yako sawasawa na matakwa ya serikali, ambapo wanataka vijana wapate umahiri pale wanapokuwa wamejifunza darasani waweze kutumia maarifa yao katika kuzalisha.

Pia amesema katika programu hiyo hadi sasa wameshiriki kwa miaka miwili na kwa mwaka huu wanapeleka vijana 32, hivyo kama chuo ushiriki wao unaanza kuchukua kasi kwa kuiunga mkono serikali na kuwa wanufaika katika mradi huo.

“Katika mradi huu wa kilimo hii ni fursa kubwa sana, katika chuo chetu tunao vijana takribani 1070, ambao wanasoma masomo ya kilimo, hivyo katika ushiriki wetu vijana wakienda kwenye mafunzo kwa vitendo wakirudi hapa tunategemea watakuwa na teknolojia ambazo zitakuwa ni za kisasa na wataweza kujiajiri, kuajiriwa na kuleta usalama wa chakula katika nchi yetu” amesema Prof. Boniface

Naye Rais wa Serikali ya wanafunzi Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Hamisi Seif, ameishukuru serikali kwa kuona ipo haja ya kuwekeza na kuthamini vijana kwa kuwawezesha kupitia mradi huo ambao vijana wengi wanaenda nchini Israel kujifunza kuhusu Kilimo.

“Hii ni fursa kwa vijana ambapo vijana wataweza kupata ujuzi ambao utawasaidia kujiajiri na kuwa na mazingira mazuri ya kuajirika pia kuongeza asilimia kubwa ya vijana ambao wanaweza wakawa nguvu kazi katika Taifa na kupunguza namba ya vijana ambao si wafanyakazi katika nchi yetu”

Mwanafunzi kutoka chuo Cha Kilimo na Mifugo Dodoma, Albogasti Mbeya amesema atayatumia mafunzo hayo kama chachu ya kuhamasisha vijana wenzake nchini kubuni njia mbalimbali ili kufanya kilimo bora kwa kutumia teknolojia za kisasa, ili kuondokana na kilimo Cha kawaida.

Mhitimu wa chuo cha Kilacha Kilimo na Mifugo, Angel Salagija amewataka vijana wenzake hasa wanawake kuchangamkia fursa za kilimo ili kujikwamua kiuchumi.

Habari Zifananazo

5 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button