VIONGOZI wa dini wametaka taifa liombewe ili mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 uwe huru, haki na amani huku Watanzania wakikumbushwa kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura.
Sambamba na hilo, Wakristo wametakiwa kuomba kwa ajili ya uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani usiwe na viashiria vinavyoweza kuhatarisha amani.
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Blaston Gavile wakati akitoa Salamu za
Krismasi kwenye ya Ibada ya Krismasi Kitaifa iliyofanyika Kanisa Kuu la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Iringa
pia alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi mzuri na kuendeleza na kuikamilisha miradi mikubwa ya
kimkakati kama Reli ya Kisasa (SGR) na Bwawa la Uzalishaji wa Umeme wa maji la Julius Nyerere.
Aidha, Askofu Gavile amewaomba Watanzania kuilinda na kuitunza miradi yote inayotekelezwa na serikali ili iwe na manufaa kwa Watanzania wote pamoja na vizazi vijavyo kwani inatumia gharama kubwa.
Vilevile, Askofu Gavile ameipongeza serikali kwa kuimarisha vifurushi vya Bima ya Afya na kuiomba serikali iangalie namna ya kuirudisha Bima ya Afya kwa Wote kwa sababu Watanzania wengi watapata changamoto katika kugharamia afya zao.
Amelitaka Kanisa kupigavita kwa nguvu zote ukatili wa aina zote akiongeza kuwa Mkoa wa Iringa unaongoza kwa ukatili kwa watoto unaosababishwa na matatizo ya ndoa.
Amewataka Watanzania kuungana kukabiliana na vitendo vya ubakaji na ulawiti ambavyo vinaenea kila siku akisema vitendo hivyo vinalifedhehesha na kulitia aibu taifa na kwamba wote wanaofanya vitendo hivyo hawana ustaarabu uliojengeka miongoni mwa Watanzania.
Naye Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa alipokuwa akihubiri katika ibada ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Azania Front, Dar es Salaam, aliwataka Wakristo kuomba kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani usiwe na viashiria vinavyoweza kuhatarisha amani.
Amesema wapo watu wasiopenda amani lakini waombaji wakiomba Mungu atadumisha amani kwa kuwa ni Mungu wa amani.
“Kupitia uchaguzi wa serikali za mitaa kulikuwa na viashiria vingi ambavyo niliviona kabisa vinaweza kuhatarisha amani kama hatutaviangalia kwenye uchaguzi ujao lazima waombaji tuombe kwa sababu huyu Bwana tuliyenaye anayezaliwa ni Bwana wa amani,” amesema.
Amesema Tanzania imepita katika kipindi kigumu cha hofu ya watu kutekwa na kwa maombi Mungu amekiondoa
kipindi hicho.
Dk Malasusa amesema mara nyingi akifungisha ndoa, amekuwa akiwaambia watu kwamba wengi ndoa zao zimeharibiwa na wasimamizi wa ndoa kwa sababu wao ni binadamu lakini wakimkaribisha Mungu katika ndoa zao
atawashauri jinsi ya kwenda katika ndoa.
“Kuna mambo mengi yanapita ndani ya familia sasa, vijana wengi hawapendi kusali lazima tumwite Mungu alete njaa na kiu ya vijana wetu kuja kusikia neno la Mungu vinginevyo makanisa yatakuwa ni ya wazee kama yalivyo katika nchi zingine,” amefafanua.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKK) Usharika wa Kijitonyama, Eliona Kimaro
amesisitiza haki itendeke katika uchaguzi mkuu wa mwakani ili kudumisha na kulinda amani iliyopo nchini.
Pia, amesema amani na haki vina uhusiano hivyo kusipokuwepo na haki hata amani haitakuwepo.
Mchungaji Kimaro amesema hayo jana wakati wa Ibada ya Sikukuu ya Krismasi ya kukumbuka kuzaliwa kwa Yesu Kristo iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kijitonyama.
“Mwakani tutakuwa na uchaguzi mkuu wa serikali na na chaguzi mbalimbali za wabunge na ngazi mbalimali za serikali lakini hamasa tunayohamasisha nchi yetu ni kutenda haki, uchaguzi uwe wa haki ili amani iendelee
kuwepo katika nchi yetu,” amesema.
Ametoa wito kwa viongozi wote duniani kutenda haki katika uongozi ikiwa ni pamoja na kusimamia katika haki ili
kudumisha amani.
Kwa upande wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kassala amewataka viongozi waliopewa nafasi
mbalimbali kutumia sikukuu ya Krismasi kuzaliwa upya kwa kujifunza kuongoza kwa kiasi kuepuka uasi.
Askofu Kassala amesema hayo katika maadhimisho ya Misa Takatifu ya Mkesha wa Krismasi kwenye Kanisa kuu la jimbo Katoliki la Geita Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani.
Wakati huo huo, Viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Morogoro wamewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani na utulivu ulipo hasa wakati wa uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na urais unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025.
Wamesema hayo kwa nyakati tofauti wakati wa mahubiri kwenye ibada ya kuadhimisha Kumbukizi ya kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristo (Krismasi).
Walisema kuwa mwaka 2025, Taifa linaingia katika uchaguzi mkuu na wito wao kwa Watanzania ni kwamba
hakuna kitu kizuri chenye baraka ya Mungu anachokipenda na kukitamani ni kuona kuwa uchaguzi huo unakuwa
wa amani.
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo katika Usharika wa Kilakala, Dk George Pindua alisema kuwa kwneye uchaguzi huo Watanzania wanahitaji kuwapata viongozi wenye maarifa, uwezo wa kuifanya nchi yetu daima iwe ni sehemu ya amani.
Kwa upande wake, Askofu Jacob Ole Mameo akitoa mahubiri katika ibada iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Bungo, ameomba serikali kuangalia mapungufu yaliyojitokeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa na kuyafanyia marekebisho ili yasijirudie.
Imeandikwa na Yohana Shida (Geita), Lydia Inda, Selemani Nzaro na Shakila Mtambo (Dar), John Nditi (Morogoro).