Vita dhidi ya mifuko ya plastiki kuanza tena leo

MSAKO wa kukamata mifuko ya plastiki katika masoko jiji la Dar es Salaam unaanza leo.

Wiki iliyopita Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla alitoa agizo hilo kwa viongozi wa masoko kutekeleza agizo la Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.

Makalla aliwaeleza viongozi hao wa masoko Dar es Salaam mwaka 2019 serikali ilizuia uzalishaji, usambazaji na uuzaji wa mifuko ya plastiki lakini watu wameanza tena kuitumia.

Alisema mifuko hiyo ina athari kwa mazingira, kwa afya na uchumi hivyo akaagiza ufanywe msako kukamata viwanda bubu mkoani humo.

Makalla alisema mifuko hiyo inazalishwa kiholela hivyo hailipiwi kodi na walioruhusiwa kuizalisha mifuko mbadala wanafunga viwanda kutokana na kuwepo utitiri wa mifuko ya plastiki.

Aliwaagiza maofisa masoko watoe taarifa za kila siku kwa wakurugenzi kwa ajili ya kuripoti mwenendo wa mifuko hiyo.

Mwenyekiti wa Soko la Tazara Veterani, Daniel Mlangu alisema amelipokea agizo hilo yuko tayari kwa ajili ya kutekeleza.

Wiki iliyopita Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo alisema tangu serikali izuie matumizi ya mifuko ya plastiki, kumekuwa na mafanikio lakini sasa tatizo limeanza kurudi.

Dk Jafo alisema hayo wakati wataalamu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) walipokutana kujadili utekelezaji wa sheria ya mazingira.

“Katika utunzaji wa mazingira dunia ilikumbana na changamoto kubwa sana ya mifuko ya plastiki na kutokana na changamoto hiyo, tukiwa na mkakati mkubwa wa kuja na Kanuni ya Sita ya Mwaka 2019 kwa lengo la kutokomeza mifuko ya plastiki”alisema na akaongeza;

“Hata hivyo, sheria ilitoa unafuu kwa kuruhusu vifungashio ili kuwasaidia wajasiriamali wadogo ambao wanafunga karanga, ubuyu na tambi, lakini imejitokeza changamoto kwa baadhi ya watu wasio waaminifu wamegeuza vifungashio kuwa vibebeo, jambo hili limekuwa changamoto kubwa,”

Dk Jafo aliagiza ifanyike oparesheni kuhakikisha mifuko ya plastiki haionekani tena mitaani na oparesheni hiyo iguse masoko, magulio, madukani na bucha za samaki na nyama.

 

Habari Zifananazo

Back to top button