IMEELEZWA kuwa matumizi ya viuatilifu kiholela kwenye mazao vya chakula inaweza kupelekea magonjwa kwa binadamu, changamoto za kimazingira na kuuwa baadhi ya viumbe hai.
Akizungumza leo Novemba 6, kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali, mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Joseph Birago amesema viuatilifu vina maelekezo ya namna ya kuvitumia ili kuhakikisha jamii inakuwa salama.
“Mkutano huu utajadili kwa namna gani tunaweza kuifikia jamii kuhakiksha tunakuwa na matumizi bora ya viuatilifu na kuhakikisha tunakuwa na Tanzania salama,” amesema Birago.
Akizungumza katika kongamano hilo la kujadili matumizi ya viuatilifu , Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Appolinary Kamuhabwa amesema kongamano hilo litakuja na majibu ya tafiti kutoka kwa watafiti mbalimbali wameona nini kwenye matumizi ya viuatilifu .
Amesema kongamano hilo pia litapokea mapendekezo ya kupeleka Wizara ya Afya, sera zipi itumike au elimu gani inapaswa kutolewa kwa makundi mbalimbali, ikiwemo wakulima na wafugaji.
“ Tunajua pia kuna mabadiliko ya tabia ya nchi, hii tunaona wadudu wanabadilika magonjwa ya mazao, wanyama na binadamu yanabadilika, baadhi ya haya magojwa yanatibia na viuatilifu sasa isipokuwa sahihi vinaenda kupata muingiliano wa viuatilifu na mabadiliko ya tabia nchi,” amesema Profesa Kamuhabwa.
Mtafiti wa magonjwa ya mimea, Vera Ngowi amesema kongamano hilo pia litajadili madhara ya viuatilifu kwa afya ya binadamu.
Amesema uchumi unavyokuwa na madhara ya afya yanaongezeka, na madhara ambayo yatajadiliwa kwenye kongamano hilo ni kisukari, presha na saratani. Amesema haya yote yanahusishwa na viuatilifu .
“Udhibifi wa viuatilifu umekuwa hafifu baada ya sheria kubadilika na hatujui nani anafanya tafiti za viuatilifu kwahiyo tunakutana leo kujadili hilo,” amesema mtafiti huyo.