VSO wajipanga kusaidia wanawake

VSO wajipanga kusaidia wanawake

SHIRIKA la Kujitolea la Kimataifa (VSO-Tanzania) mkoani Geita limeweka mikakati ya kukuza uwezeshaji wanawake katika matumizi ya majukwaa ya kidijitali ili kusaidia kufikiwa kwa azma ya maendeleo endelevu.

Mtaalamu wa Masuala ya Kijinsia na Ujumuishi kutoka VSO, Hellen Mahindi ametoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwenye Halmashauri ya Mji wa Geita.

Hellen alisema kujenga uwezeshaji  wa mfumo wa kidijitali kwa vikundi vya wanawake kunalenga kuongeza uelewa kuelekea usimamizi ufaao na ufuatiliaji wa fursa mbalimbali za maendeleo.

Advertisement

Alieleza mpango huo ni sehemu ya mradi wa Pamoja wa Utekelezaji wa Haki katika Sekta ya Uziduaji (CLARITY), unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kulenga kuwainua wanawake kiuchumi, kijamii na kisiasa.

“Tumewekeza kwenye mifumo ya kidijitali kwa sababu hapa ndipo dunia ilipo, na katika kuwakomboa wanawake kiuchumi, unaweza kutumia mitandao ya kijamii kama jukwaa la kutangaza bidhaa zao,” alisema.

Alisema mpango huo hautasaidia tu walengwa kuendesha shughuli zao kidijitali, bali pia kutumia mitandao ya kijamii kuhamasisha kampeni za kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Geita, Zahra Michuzi alisema halmashauri imefanikiwa kuunda jumla ya kamati 92 za ulinzi wa wanawake na watoto, ili kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Alifafanua, kamati 78 zipo katika ngazi ya vijiji na mitaa, kamati 13 za kata na kamati moja ya halmashauri na zimepatiwa mafunzo kamili ya masuala ya jinsia, ili kukomesha ukatili wa kijinsia.

“Ili kuwawezesha wanawake, jumla ya vikundi vya wanawake 668 vimesajiliwa na kupata cheti, huku vikundi 468 vyenye wanachama 2,340 vimenufaika na mkopo usio na riba wenye thamani ya Sh bilioni 2.26 kuanzia mwaka 2017 hadi 2023,” amesema.

Mbunge wa Jimbo la Geita mjini, Costantine Kanyasu alitaka mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na taasisi za umma kufanya kazi kwa ushirikiano katika masuala ya jinsia, ili kufikia sera ya usawa wa kijinsia.