HAITI : UMOJA wa Mataifa umeonya kuhusu ongezeko la mashambulizi dhidi ya vyombo vya habari nchini Haiti, akisema kuwa vyombo hivyo vinalengwa na magenge ya wahalifu yanayojaribu kuvinyamazisha. Shirika hilo limetaja hali hiyo kama tishio kwa uhuru wa vyombo vya habari na usalama wa waandishi wa habari katika taifa hilo la Karibiani.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini Haiti, Eric Voli Bi, amesema kuwa mazingira ya kufanya kazi kwa waandishi wa habari nchini humo ni magumu na yanatia wasiwasi. Alisema kwamba vyombo vya habari vimekuwa vikilengwa na baadhi ya magenge ya wahalifu na hata kuteketezwa kabisa.
Desemba mwaka jana, waandishi wawili wa habari walipigwa risasi na kuuawa katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, walipokuwa wakiripoti kuhusu kufunguliwa tena kwa hospitali. Tukio hili limetia wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa waandishi wa habari katika nchi hiyo, huku hali ya ghasia ikiongezeka.
Vilevile, wiki iliyopita, ofisi za kituo cha televisheni pamoja na vituo viwili vya redio vilishambuliwa na kuporwa na wahalifu. Mashambulizi haya yanaonyesha wazi kiwango cha hatari wanachokabiliana nacho waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini Haiti.
Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa hatua za haraka zinahitajika ili kulinda uhuru wa vyombo vya habari na kuhakikisha usalama wa waandishi wa habari, ambao wanachukua jukumu muhimu katika kutoa habari kwa umma na kudumisha uwazi katika jamii.
SOMA: Alix Didier waziri mkuu mpya Haiti