ASKARI wa usalama wa Uganda wamewakamata watu kadhaa waliojaribu kuandamana kwenda majengo ya bunge kupinga kiwango kikubwa cha rushwa, maandamano ambayo serikali ya nchi hiyo imesema ni kinyume cha sheria.
Idadi kubwa ya polisi na wanajeshi waliweka doria sehemu mbalimbali za mji mkuu, Kampala ambako makundi madogo ya waandamani walikusanyika.
Maandamano hayo yaliandaliwa na raia wa Uganda wenye tumaini la kuiga juhudi za watu wa nchi jirani ya Kenya, ambao hivi karibuni maandamano yao mitaani yalimlazimu Rais William Ruto kuvunja baraza karibu lote la mawaziri baada ya muswada wa sheria ya fedha uliowasilishwa bungeni kupingwa kwa kiasi kikubwa.
“Tumelinda mwelekeo wa njia ya mapinduzi ya Uganda hapo awali na tutailinda zaidi sasa,” Museveni alisema katika hotuba iliyorushwa kwenye televisheni Julai 20, akionya waandaaji wa maandamano kwamba walikuwa “wanacheza na moto.”
Waganda wana hasira kutokana na madai ya kuongezeka kwa rushwa dhidi ya Spika wa Bunge, Anita Among, ambaye amekataa wito wa kujiuzulu.
Kampeni ya kupambana na rushwa ilianza kwa kufichuliwa mtandaoni kwa madai ya matumizi yasiyo ya kawaida ya ofisi ya spika na wengine walio karibu naye.
Rais Museveni amekuwa madarakani tangu 1986, na serikali yake mara nyingi imekuwa ikidaiwa kuwalinda viongozi wala rushwa.
Licha ya ahadi yake kukomesha rushwa baada ya kuchaguliwa tena mwaka 2021, wananchi wengi wa Uganda bado hawana imani.
Vyombo vya habari vya Uganda mara kwa mara huripoti vitendo vya rushwa lakini wanaharakati na viongozi wa upinzani wanaojaribu kupinga hukamatwa kutokana na sheria inayowataka kutoa taarifa mapema kwa polisi.