Wabunge washauri njia za kuongeza kasi uchumi

DODOMA – WABUNGE wameishauri serikali izingatie kuboresha kilimo, elimu na mazingira ya biashara kama njia za kuongeza kasi ya kukuza uchumi.

Walisema hayo bungeni Dodoma wakati wakichangia mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo alisema ni muhimu kuzingatia mambo hayo wakati wa kuandaa dira mpya ya maendeleo ya 2025- 2050 sanjari na kujiuliza nchi zilizokuwa na uchumi sawa na Tanzania katika miaka ya 60’s zilifanya nini kufika zilipo sasa.

Profesa Muhongo alisema ili uchumi ukue kwa kati ya asilimia nane hadi 10, lazima kuboresha elimu katika ngazi zote, kuwe na nishati ya uhakika kwa bei nafuu, bidhaa bora na nyingi kupelekwa katika soko la dunia itakayokuwa na takribani watu bilioni 10 ifikapo mwaka 2050.

Alihimiza kilimo cha umwagiliaji mazao yenye soko kubwa duniani hasa mchele, ngano, viazi mviringo, mahindi, mihogo, maharage, soya, korosho na matunda.

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku Musukuma amehimiza serikali isikilize na itatue changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wakiwemo wa Kariakoo mkoani Dar es Salaam.

“Tukiiua Kariakoo tutakuja kushikana mashati humu ndani, Kariakoo ndio kila kitu kwa Tanzania kwa hiyo ni vizuri tupalinde…kamatakamata Kariakoo ni nyingi mno, hakuna mgeni anaenda kwenye nchi inayokamata, ukinunua katisheti unapini, ukinunua haka unapini..,” alisema Musukuma.

 

View this post on Instagram

 

A post shared by HABARILEO (@habarileo_tz)

Aliongeza: “Wazambia sasa hivi wanaenda Uganda, tuiangalie Kariakoo tusije tukaipoteza tutapata hasara kubwa, ni vizuri muwasikilize, kama wana mambo yao wasikilizeni”.

Pia Musukuma aliihimiza serikali iharakishe kasi ya kuandaa muswada wa marekebisho ya sheria ya sukari ili kumaliza changamoto ya upatikanaji wa bidhaa hiyo kila mwaka.

Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage ameipongeza serikali kwa kutilia mkazo ujenzi wa viwanda vidogo vijijini kwa kuwa vitajenga utamaduni kwa Watanzania waache kwenda mijini na wapate mwamko wa kumiliki viwanda vikubwa.

Pia Mwijage amehimiza kuboresha mazingira ya biashara ikiwemo ya kilimo cha mpunga ikiwa ni pamoja na kuondoa kodi zuio ili biashara hiyo ifanywe kwa uwazi na serikali ipate mapato.

Ameishauri serikali ifikirie upya na iondoe tozo kwenye gesi ya magari ili Watanzania wengi waitumie na kuihakikishia nchi usalama wakati wa tatizo la mafuta.

SOMA: Paroko, baba mbaroni mauaji ya Asimwe

Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Tendegu alihimiza yajengwe mazingira mazuri ya kuwezesha wananchi kutumia gesi kwenye magari. Tendegu alisema jambo hilo muhimu kwa kuwa gesi inayotumika inapatikana nchini hivyo itapunguza matumizi ya Dola za Marekani kuagiza mafuta.

Alisema ameshtushwa na pendekezo la serikali kuweka tozo ya Sh 382 kwa kila kilo ya gesi na akasema jambo hilo si sawa kwa kuwa litawavunja moyo waliohamasika kutumia gesi kwenye magari.

“Tunatakiwa tuweke ruzuku kwa ajili ya vifaa vya kuweka kwenye magari ili wananchi waweze kuweka kwa gharama ndogo au kama ni ruzuku basi waweke kwanza ili gesi yetu iweze kutumika na inunulike itumike vizuri,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button