Wabunge wataka fedha za mikopo ya ardhi zirejeshwe

WABUNGE wamehoji utekelezaji wa Mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha (KKK) na kuitaka serikali isimamie na kuratibu urejeshwaji wa mikopo kutoka halmashauri zilizopata kutekeleza jukumu hilo.

Hayo yamebainishwa jana wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/2024 yaliyowasilishwa jana bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika maoni yake, ilisema kamati imebaini serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imepeleka katika baadhi ya halmashauri Sh bilioni moja kama mkopo kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi.

Advertisement

Mwenyekiti wa kamati, Dennis Londo alisema hata hivyo, imebainika kuwa halmashauri nyingi zilizopata mkopo huo zimeshindwa kurejesha mkopo na haziendelei tena na shughuli za kupima viwanja.

Alisema kutokana na hali hiyo, eneo kubwa la ardhi katika halmashauri nchini linaendelea kubaki bila kupimwa, hali inayosababisha migogoro ya ardhi miongoni mwa jamii kuendelea kuwepo.

“Serikali isimamie na kuratibu urejeshwaji wa mikopo hiyo kutoka halmashauri zote zilizopata mkopo huo,” alishauri Londo na kutaka pia serikali kufanya tathmini ya matumizi ya mkopo huo na mafanikio katika upimaji wa ardhi za halmashauri.

Ushauri mwingine wa kamati ni kwamba, serikali iratibu mapato yatokanayo na uuzwaji wa ardhi iliyopimwa kuendelea kutumika kupima maeneo mengine. Awali, Kairuki alisema Ofisi ya Rais -Tamisemi kwa kushirikiana na wizara za kisekta, taasisi na wadau wengine inatekeleza mradi huo wa KKK katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na kwamba halmashauri 55 zilipata mkopo wa jumla ya Sh bilioni 49.47.

Alisema mradi umeleta mafanikio makubwa ya kuwezesha kupima jumla ya viwanja 232,537 sawa na asilimia 91.73 kati ya lengo la viwanja 253,500 na hivyo kusaidia kupunguza tatizo la uendelezaji holela wa ardhi kwenye maeneo ya miji husika. Kwa mujibu wake, hadi Februari 2023, jumla ya Sh bilioni 16.75 sawa na asilimia 33.85 ya fedha zilizotolewa zimerejeshwa.