Wachimbaji wadogo Geita waja kivingine
GEITA; CHAMA cha Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Geita (GEREMA), kimekuja na mikakati mipya kuwezesha sekta ya madini inaendelea kupiga hatua zaidi na kuongeza mchango kwenye maendeleo ya taifa.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni kumaliza migogoro ya wachimbaji wadogo, kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme migodini, maboresho ya huduma za maji na miundombinu ya barabara na utafiti wa madini.
Hayo yameelezwa na viongozi wapya wa wachimbaji wadogo ngazi ya wilaya na mkoa mara baada ya uchaguzi uliofanyika mjini Geita mkoani hapa.
Mwenyekiti wa Gerema, Titus Kabuo amekiri shida kubwa iliyopo migodini inatokana na migogoro baina ya wachimbaji wenyewe ama wachimbaji na wamiliki wa ardhi hivo ni lazima ikomeshwe.
“Yote hayo yanaweza yakatatuliwa kwa njia ya mazungumzo, mimi naamini zaidi kwa njia ya mazungumzo, tukikaa mezani tutatatua,” amesema na kuongeza;
“Tutahakikisha tunaenda kuwa mwarobaini wa yale matatizo madogo madogo ya wachimbaji kwa sababu kama ni suala la leseni, serikali imelidhibiti, na wachimbaji wanapata leseni,” amesema Kabuo.
Ameeleza pia wamejipanga kuhakikisha wanasimamia upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa wachimbaji wadogo, kwani sasa wanafanya kazi kwa uhakika na kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wilaya ya Nyanghwale, Misana Jeremiah amesema wamejipanga kushirikiana na serikali kuhakikisha wachimbaji wadogo wanafuata taratibu, kanuni na sheria za madini.
Makamu Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wilaya ya Bukombe, Sangudi Hamis amesema msingi mkubwa wa kumaliza migogoro kwa wanachama wao ni kusimamia sheria zilizowekwa na Gerema.
Isome pia: ‘Mikakati sita kuinua wachimbaji wadogo’
Naye Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wilaya ya Mbogwe, Dwasi Sumuni amesema watashirikiana na wachimbaji kuwezesha upatikanaji wa leseni kwa maeneo yaliyo wazi bila upendeleo wa kundi fulani.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Gerema, Mwakilishi kutoka Shirikisho la Wachimbaji Wadogo (FEMATA), David Bitta ameagiza kila wilaya iwe na ofisi za wachimbaji wadogo ili viongozi wafikiwe kwa urahisi.
Bitta amewaomba viongozi kuwekeza muda wao katika kujenga umoja na mshikamano, kuvunja makundi, kutoa elimu kwa wachimbaji pamoja na kuwashika mkono wachimbaji wasio rasmi.